September 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaharakati walaani kuchapwa viboko wanawake Tabora

Na Penina Malundo,timesmajira

MTANDAO wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi imelaani vikali kitendo cha wanawake wakongwe wilayani urambo mkoani Tabora kuchapwa viboko ni kutokuheshimu utu wa mwanamke na kutumia  matumizi mabaya ya mamlaka ambayo ni  kinyume na Katiba na Sheria za Tanzania.

Pia wametoa wito kwa  Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ,Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pamoja na  Jeshi la Polisi Tanzania kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kufanya upelelezi kwa wale wote waliohusika katika tukio hilo la kinyama na la kusikitisha, kuwarejesha wanawake hao katika makazi yao pamoja na kuwapatia ulinzi. 

Tamko lilitolewa leo na Mtandao huo ambao unawanachama zaidi ya 50 umesema katika Ibara ya 12(i)i[i] ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasisitiza kuwa kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. 

Umeswma pia, ibara ya 13(i)ii[ii] imeainisha umuhimu  wa usawa na haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria na nchi ya Tanzania  inatambua na kutekeleza maazimio ya Tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambalo linasisitiza chini ya Ibara ya 3 haki ya kuwa huru na kulindwa.

“Kitendo cha kujichukulia sheria mkononi, kujeruhi na kusababisha madhara ni kosa la jinai sawasawa na  kifungu cha  225 na kifungu cha 228(a) cha sheria ya Kanuni ya Adhabu/ Penal Code [CAP. 16 R.E. 2022] na kanuni ya  maadili ya madiwani zimeweka bayana umuhimu wa kuheshimu na kuzingatia sheria kwa madiwani ikiwa ni pamoja na kuendesha shughuli zao kufuatana na dhamana waliyopewa na wananchi,”umesema mtandao huo.

Aidha Mtandao umeendelea kutoa wito kwa jamii kutovifumbia macho vitendo dhalilishi, vya kikatili, vya kinyama na vya uvunjifu wa haki kwa wanawake na jamii nzima kuchukua hatua na kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi vitendo hivyo vinapofanyika.

Mtandao umesema ukatili wa kijinsia haukubaliki wakati wowote na mtu yeyote awe kiongozi ama raia wa kawaida, uthubutu wa kuendelea kufanya vitendo hivi hususan katika kipindi hiki cha kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia vinakasirisha na kukera na vinaonyesha upungufu wa maadili na uvunjwaji wa sheria ambao unafifisha jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali pamoja na wadau wa masuala ya haki za wanawake na binadamu kwa ujumla.

Chanzo cha  tukio hilo kinaonyesha kuwa Mwanamke mmoja ametoa taarifa kuwa yeye, pamoja na wanawake wengine watatu na binti zao wawili mmoja akiwa mjamzito, wamechapwa viboko wakiwa wamemwagiwa maji na kupunguzwa nguo mwilini. 

Kitendo hicho kimefanywa na Diwani wa Kata ya Kasisi, Wilaya ya Urambo, Mkoa wa Tabora kwa madai kuwa wanawake hao ni wachawi na washirikina ambao wamekuwa wakichukua vyakula vya watu kwa nguvu za kishirikina wakati wa usiku.

 Wanawake hao walipatwa na kadhia hiyo wakiwa katika shughuli zao za kujipatia kipato ambapo kufuatia tukio hilo walipoteza mazao na vitu mbalimbali ambapo  tukio hilo  liliwasababishia maumivu makali ya mwili na viungo,limewadhalilisha wao binafsi, familia zao na jamii nzima.