January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB Kinara wa usawa wa kijinsia Afrika

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Ubaguzi wa kijinsia ni mwiko kwa Benki ya NMB na juhudi zake za kutokomeza kabisa unyanyapaaji huo nchini zimeiheshimisha duniani na kupelekea harakati zake za kupambania usawa wa kijinsia kazini kuthibitishwa rasmi kimataifa.

Benki hiyo imetunukiwa na taasisi ya The Edge Certified Foundation hati maalumu ya kutambulika rasmi duniani kama kinara katika mgawanyo wa kiuchumi kwenye suala la kijinsia (EDGE Certification) miongoni mwa taasisi za kifedha barani Afrika.

NMB ni ya kwanza kupata mafanikio hayo kitaasisi kwenye nchi zote zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara. Bw Akonaay alisema zipo taasisi nyingine mbili ambazo si za kifedha zenye hati hiyo za Kaskazini mwa Afrika (Moroco na Misri).

Aidha, tafiti zimedhibitisha kuwa uwiano wa kijinsia ni kichocheo kizuri cha ubunifu na ukuaji wa kiuchumi, kuimarika kwa shughuli za uzalishaji mali na kuwepo utulivu wa kifedha na uwiano wa kipato.

Pia NMB inatambua kuwa swala hili ni miongoni ya vipaumbele vya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa. Bw Akonaay alisema umuhimu wake kimaendeleo ni pamoja na kuzingatia ukuaji wa biashara za kibenki.

Alibainisha faida nyingine za cheti cha EDGE Access ambayo ni hatua ya kwanza ya taasisi kuelekea kufanikiwa kuutokomeza kabisa ubaguzi wa kijinsia ni pamoja na NMB kutambulika kama muajiri anayezingatia masuala ya usawa wa kijinsia kazini.

Naye, Mwakilishi wake mkazi, Bw Frank Ajilore, alisema usawa wa kijinsia kazini kuna faida nyingi kibiashara na kiuchumi kwani akina mama wakiwezeshwa wanachangia vizuri kasi ya maendeleo.

Benki ya NMB yenye wafanyakazi zaidi ya 3,500 imepiga hatua kubwa kwenye eneo hili na uwiano wake wa kijinsia umepanda kutoka asilimia 45 wanawake na asilimia 55 wanaume mwaka 2015 hadi asilimia 48 kwa 52 mwaka huu.

Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay (katikati) na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la IFC, Frank Ajilore (wapili kulia) wakionyesha hati ya kutambulika ya Uimara wa Kiuchumi na Usawa wa Kijinsia iliyotolewa kwa benki ya NMB na taasisi ya The EDGE (Economic Dividends for Gender Equality) Certified Foundation. Hafla hiyo ya makabidhiano ilifanyika jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mkuu wa masuala Jinsia wa IFC Afrika, Anne Kabugi, kushoto ni Afisa Mkuu Huduma Shirikishi wa NMB, Nenyuata Menjooli na wapili kushoto ni Afisa Mkuu wa Udhibiti NMB, Doreen Joseph