November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BREAKING NEWS:Maafisa wa Kenya wawagomea madereva wa Tanzania kuingia nchini humo, wadai hawaviamini vyeti vya Tanzania kuhusu Corona

Na Heckton Chuwa, TimesMajira Online

Licha ya viongozi wa Tanzania na Kenya kukutana hivi karibuni kutatua changamoto ya usafiri unaohusisha madereva wa masafa marefu wa nchi hizo bado hali ni tete katika mipaka ya nchi hizo mbili iliyoko wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kwa upande wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana wilayani Rombo bado madereva wa pande zote mbili wamekwama maeneo ya mipaka miwili ya Tarakea na Holili iliyoko wilayani humo kutokana na kutokuelewana na kuhusiana na vibali vinavyothibitishwa madereva kuwa wamepimwa na hawana virusi vya Corona.

Akidhibitisha kuwepo kwa sintofahamu hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agnes Hokororo amesema kuwa, imebidi hali iwe hivyo baada ya wenzao wa Kenya kukataa kata kata vyeti vya uthibitisho wa madereva wa Tanzania.

“Madereva wetu wamezuiwa na maofisa wa Kenya kwa vile hawana vyeti vya uthibitisho vinavyohusiana na hali za za kiafya inayohusiana na ugonjwa wa Corona kutoka Kenya, vile vya Tanzania hawavitaki. Ila wao wanataka madereva wao ambao wanavyeti kutoka nchini kwao, lakini hawana vya kwetu wapite tu, sasa itakuwaje hivyo wakati wao vya kwetu hawataki? Na wao imebidi wabaki huko kwao,”amesema.

Hokororo amesema kuwa, pamoja na wao viongozi wa Tanzania kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa Arusha, wenzao wa Kenya hawajaoneyesha utayari wa kuheshimu makubaliano hayo.

“Sisi tunajali na kuheshimu ujirani mwema, tumezungumza na wenzetu na kuwakumbusha kuwa muafaka kuhusiana na suala la madereva ulishapatikana Arusha na kwamba tulipata muongozo wa makubaliano hayo kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, lakini wao walikataa na kusema kuwa maagizo waliyonayo kutoka kwa viongozi wao ni kuwa waruhusu madereva kutoka Tanzania ambao wana vyeti wa vya uthibitisho kutoka Kenya tu na si vinginevyo,”amesema.

Amesema kuwa, hali hiyo inaonekana kuwa mbaya zaidi kwenye mpaka wa Holili kutokana na ukweli mpaka huo unatumika kwa saa 24 tofauti na ule ulio eneo la Tarakea ambao hutumika wakati wa mchana tu, saa za kazi.