October 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Barabara ya Tanga–Segera kufungwa kwa muda kesho

*TANROADS kufanya ukarabati wa madaraja ya Hale na Maguzoni

*Magari madogo yaelekezwa njia mbadala kuepuka usumbufu

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amewataka watumiaji wa barabara ya kimataifa ya Tanga–Segera kupanga safari zao mapema. Amewataka kuzingatia tahadhari zilizotolewa na Serikali kufuatia kufungwa kwa muda kwa njia hiyo kesho, Oktoba 20, 2026.

Hatua hiyo inatarajiwa kuchukuliwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana. Lengo ni kumpa mkandarasi nafasi ya kufanya ukarabati wa madaraja ya Hale na Maguzoni kwa usalama na ufanisi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt. Batilda amesema kufungwa huko ni hatua muhimu katika kuwezesha uboreshaji wa miundombinu hiyo. Amewasihi madereva, wafanyabiashara, wachukuzi na wasafiri wengine kupanga shughuli zao vizuri ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Amesema njia hiyo ina umuhimu mkubwa kiuchumi na kijamii kutokana na kutumika kusafirisha abiria na mizigo. Pia, inaunganisha maeneo mbalimbali ya nchi na nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kutokana na umuhimu huo, amesisitiza wananchi kupata taarifa sahihi na za mapema ili wafanye maandalizi yatakayowasaidia kuendelea na shughuli zao kulingana na hali itakayokuwepo. Ushirikiano wao ni muhimu katika kuhakikisha zoezi hili linafanyika bila changamoto kubwa.

Aidha, ameeleza kuwa tahadhari hii inatolewa katika kipindi ambacho wataalamu wa hali ya hewa wameonya kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mvua za El Niño. Hali hii inahitaji maandalizi ya mapema na umakini mkubwa kwenye sekta ya usafiri.

Mkuu huyo wa mkoa amewataka madereva kutokulazimisha kupita katika maeneo yaliyofungwa na badala yake kufuata maelekezo ya askari. Ili kudhibiti msongamano, amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, SACP Almachius Mchunguzi, kuimarisha ulinzi na usimamizi wa usalama barabarani.

Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wanapaswa kutoa taarifa mapema na kuhakikisha alama za tahadhari zinawekwa. Hatua hii itawawezesha wasafiri kutambua vizuizi na kufanya maamuzi sahihi kabla ya kufika kwenye maeneo ya kazi.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama K. Msama, amesema kuwa magari madogo yatakuwa na uwezekano wa kutumia njia mbadala kutoka Tanga kupitia Maguzoni, kisha kuelekea Mnyuzi na Rwengera kabla ya kuendelea na safari kuelekea Korogwe.

Mhandisi Msama amebainisha kuwa utaratibu huo unalenga kupunguza usumbufu kwa watumiaji wa usafiri huo, huku magari makubwa yakishauriwa kusubiri hadi kazi zitakapokamilika. TANROADS itahakikisha mkandarasi anakuwa na vifaa vyote vinavyohitajika kwa wakati ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Naye Kamanda Mchunguzi amesema Jeshi la Polisi litahakikisha askari wanawekwa pande zote za Segera na Maguzoni kutoa maelekezo na kudhibiti mtiririko wa vyombo vya moto. Amesitiza kuwa ushirikiano wa madereva ni jambo la msingi wakati ukarabati huo ukiendelea.