Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga
Umoja wa wamiliki na waendesha pikipiki na bajaji wilaya ya Tanga Mjini (UWAPIBATA) Umempongeza Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa hatua madhubuti anazochukua kuhakikisha kuwa ongezeko la bei ya mafuta kwenye soko la dunia hazileti athari kubwa katika maisha ya wananchi na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
Hatua hizo ni pamoja na kuweka ruzuku ya shilingi bilioni 100 ambayo kila mtu amejionea jinsi ambavyo imesaidia kupunguza bei za petrol na dizeli nchi nzima kuanzia tarehe 1 juni.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa kikao cha waendesha pikipiki na bajaji kilichoshirikisha viongozi wa jeshi la polisi akiwemo kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Leopord Fungu kilichoketi jijini Tanga.
Awali akisoma taarifa kwa vyombo vya habari jijini Tanga Mwenyekiti wa umoja wa wamiliki na waendesha pikipiki na bajaji Wilaya ya Tanga Mjini Mohamed Chande wao umoja wa wamiliki na waendesha pikipiki na bajaji wanaunga mkono juhudi za Rais Samia za kudhibiti ongezeko la bei ya mafuta.
“Tunampongeza kwa uongozi wake mahiri na shupavu na kumtaka aendelee “kuupiga mwingi” katika jitihada zake za kuleta maendeleo nchini, “alisisitiza Chande.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati (EWURA) , ruzuku ya shilingi bilioni 100 ya Rais Samia imesaidia kupunguza bei ya mafuta ambapo kwa bandari ya Tanga, petroli imeshuka kwa shilingi 152 kwa lita na dizeli imeshuka kwa shilingi 476 kwa lita.
“Kabla ya ruzuku ya Rais Samia ya shilingi bilioni 100 sisi wamiliki na waendesha pikipiki na bajajo Mkoani Tanga tulikuwa tunanunua petrol kwa shilingi 3137 kwa lita lakini kwa sasa bei hiyo imeshuka hadi kufikia shilingi 2985 huku kila lita moja ya petrol ikiwa na ruzuku ya shilingi 152.
Chande alisema kwa upande wa dizeli lita moja iliuzwa iliuzwa kwa shilingi 3639 kwa lita kabla ya ruzuku ya Rais Samia na sasa inauzwa kwa shilingi 3162 kwa lita ikiwa kila lita moja ya dizeli imewekewa ruzuku ya shilingi 476.
“Wamiliki na waendesha pikipiki na bajaji wilaya ya Tanga mjini tunampongeza Rais Samia na serikali anayoiongoza kwa kutujali sisi wananchi na kuweka ruzuku hii kubwa kwenye bei za petrol na dizel nchini,! Alisisitiza Chande.
Alisema Ruzuku ya Rais Samia kwenye mafuta imeleta ahueni kwao wamiliki na waendesha pikipiki na bajaji kwani imesaidia kupunguza ugumu wa maisha kwa kushusha gharama za uendeshaji wa pikipiki na bajaji.
“Tunatoa wito kwa serikali ichukue hatua za kikodi kwenye bajeti kuu ya serikali itakayosomwa bungeni mwezi huu ili kupunguza zaidi bei za petrol na dizeli kuanzia mwaka ujao wa fedha wa 2022/23 unaoanza julai 1.
Kwa upande wake kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa Tanga Leopord Fungu amewataka bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani wakati wanapoendesha vyombo vya moto.
Kamanda Fungu pia amewataka bodaboda wanaotembea bila vioo vya pikipiki kuacha tabia hiyo mara moja kwa kild alichodai ni miongoni mwa vyanzo vinavyosababisha ajali.
Pia amewataka kuachana na ubebaji wa mishikaki au bajaji kubeba idadi kubwa ya watu tofauti na inavyotakiwa na kwamba watakaofanya hivyo watakutana na mkono wa sheria.
Pikipiki na bajaji hutumika kusafirisha abiria mbalimbali ikiwemo wafanyakazi, wakulima, wwaavuvi, wafanyabiashara na pia kubeba mizigo na hata wakati mwingine kubeba wagonjwa kuwapeleka hospitali.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â