Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
IMEELEZWA kuwa wagonjwa wengi wa saratani wanafika katika vituo vya kutolea huduma wakiwa katika hatua mbaya,kutokana na kukosekana kwa taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo kwa jamii.
Hivyo kupitia mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) ambao unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na Aga Khan Foundation (AKF) , waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna ya kuripoti habari zinazohusiana na ugonjwa wa saratani kwa usahihi.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza juu ya namna ya kuandika habari sahihi za afya hususani za ugonjwa wa saratani,Meneja Ubia,Uwezeshaji na Mawasiliano wa mradi wa TCCP Dkt.Sarah Maongezi amesema, miongoni mwa changamoto katika huduma za saratani nchini hapa ni pamoja na wagonjwa wengi kufika katika hospitali wakiwa katika hatua za mwisho.
Ambapo kubwa zaidi ni uelewa na elimu ndogo katika jamii juu ya saratani huku mradi huo unatarajia kuwanufaisha watu milioni 1.7, ikiwemo waandishi wa habari ambao wamewapatia elimu sahihi juu ya saratani hivyo wataweza kufikisha taarifa sahihi kwa jamii kwani inawaamini pia wanauwezo wa kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja.
“Wagonjwa wengi wa saratani wanafika katika hospitali zetu wakiwa katika hatua ya tatu na ya nne,lakini uelewa mdogo katika jamii nina hakika ninyi waandishi wa habari mnajua,pia uhaba wa mashine za tiba ya saratani kuuzwa bei ghali,kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mashine 1 inapaswa kuhudumia watu milioni Moja na hapa nchini tupo milioni 60 tuna mashine 7 tu,” amesema Dkt.Maongezi.
Daktari Bingwa wa upasuaji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, Dkt.Athanas Ngambakubi,akitoa elimu juu ya saratani kwa waandishi wa habari hao, amesema kwa mwaka 2020 inakadiriwa watu milioni 1.1 walipata saratani.
Huku watu 711,429 waliofariki kwa saratani Afrika wakati huo Tanzania watu 40,464 walipata saratani kati yao 26,945 walifariki kutokana na saratani.
“Hivyo amesema nchini hapa saratani inayoongeza ni ya mlango wa kizazi,matiti na tezi dume,hivyo katika kupambana na ugonjwa huo,wenzetu Aga Khan,wameamua kuja na mradi huo,”
Awali akifungua mafunzo hayo Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt. Beda Likonda,amesema ipo mihimili minne ambayo ikitendewa haki jamii itafikiwa na kuleta matokeo chanya ikiwemo takwimu,elimu,tiba na tiba shufaa
Dkt .Likonda amesema wanatakiwa kutoa elimu kwa jamii,wafanyakazi na wadau wa sekta ya afya,ili wajue saratani ni nini, inatokana na nini,jinsi gani ya kujizuia na je,wafanye nini na wakipata wagonjwa waweze kuwatibu.
Pia amesema,serikali ihakikishe tiba zinapatikana kuanzia katika hatua mbalimbali za vituo vya tiba kama vile vituo vya afya, zahanati,hospitali za mikoa na wilaya ili huduma ziwafikie wananchi.
Aidha amesema,mhimili wa nne ni tiba shufaa ambayo mgonjwa anarudi nyumbani hana uwezo wa kumtibu,hata kama atafariki asiwe kwenye matatizo mengi.
“Katika mihimi hiyo ya kupambana na adui yetu saratani,kuna mapungufu mengi,nimefurahi wenzetu wa Aga Khan na Wafaransa wameungana kuona tunaifikia vipi hii mihimili minne,wameanza na mihimili miwili watatusaidia katika kujenga na kuhakikisha mihili yote mine inakamilika ili tuweze kupigana vizuri na saratani (adui yetu),”amesema.
More Stories
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa