Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Mwakilagi, amemshauri Mkurugenzi wa Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), kusitisha mikataba ya Wakandarasi wa miradi ya vyoo kwenye baadhi ya shule za msingi wilayani humo.
Miradi hiyo ya ujenzi wa vyoo vya wanafunzi na walimu kwa shule za msingi wilayani humo,inatekelezwa kupitia ufadhili wa Benki ya uwekezaji ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa na kusimamiwa na MWAUWASA,ambayo imepita muda wake huku utekelezaji wake ukisuasua.
Ushauri huo ameutoa baada ya kutembelea shule za msingi Nyakabungo,Sahara na Azimio zilizopo wilayani humo,katika ziara yake ya kujionea maendeleo ya mradi wa ujenzi wa vyoo vya wanafunzi na walimu Wilaya ya Nyamagana,ambapo hakuridhishwa na kasi ya utekelezaji wake.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika shule hizo, Mwakilagi amesema, wakandarasi CF Builders ya Mwanza na GOPA Contractors Tanzania Limited ya Dar es Salaam mikataba yao inapaswa kusitishwa ili iwe fundisho kwa wakandarasi wengine ambao hawana uzalendo.
Hivyo Mkurugenzi wa MWAUWASA Mhandisi Leonard Msenyele akae na bodi ya wakurugenzi ya MWAUWASA kupitia mikataba hiyo,kushauriana na kisha kusitisha mikataba ya Wakandarasi hao ili waweze kutafuta wakandarasi wazalendo watakaomalizia miradi hiyo na watoto waweze kupata huduma ya choo.
“Mkurugenzi katika mradi huu mkae chini na menejimenti yako pamoja na bodi, tujenge hoja na haja ya kusitisha mikataba,mkiridhika na mambo ya msingi zifikishie mamlaka zinazo husika na mimi nipate nakala,na mimi ni mshauri wa Mkuu wa Mkoa wakati nyie mnapita mkono huu na sisi tunapita mkono huu,tupate majibu ya haraka,tupate mkandarasi mzalendo ambaye atakwenda na kasi yetu na ya Rais Samia,”amesema Mwakilagi.
Mwakilagi amesema,mradi ni mzuri ila mkandarasi siye,mara ya kwanza alikifika katika shule ya msingi Sahara alikuta mradi unasuasua,amerudi mara ya pili mradi bado unasuasua huku maelezo alioyatoa mkandarasi hawaridhiki nayo.
“Mimi natoa maelekezo hapa tuanzishe mchakato wa kusitisha mkataba, mkandarasi wala siyo mzalendo,maana sababu anazo zitoa hazina mashiko na ukizingatia mkataba tulio ingia naye muda wake umeisha pita kwaio yupo nje ya muda,”amesema Mwakilagi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Isamilo Charlse Nyamasiriri,amesema ujenzi wa choo katika shule ya msingi Nyakabungo,ulikuwa umesimama ila baada ya kuona ujio wa Mkuu wa Wilaya ndio wakaanza tena kutengeneza na pengine hiyo ni geresha wakiondoka wanaweza kusitisha tena.
“Mimi nimefika hapa mapema,alikuwa anaingia fundi mmoja,na hapa inawezekana ni geresha,kwenye Kata yetu tuna miradi hii mitatu ambayo nayo imesima,kuna wa shule ya msingi Lake ujenzi wake haujawai kuanza kabisa, kwaio utaona namna gani hii miradi inavyoenda taratibu sana,ni bora watu wawe wanasema ukweli kwamba kuna changamoto sehemu fulani,”amesema Nyamasiriri.
Kwa upande wake Meneja Miradi wa MWAUWASA Gogadi Mgwatu,amesema Mkandarasi wa GOPA Contractors Tanzania Limited ya Dar es Salaam,yeye alipewa mkataba wa kujenga vyoo katika shule 11 wilayani Nyamagana kwa gharama ya bilioni 1.5 huku Mkandarasi
CF Builders ya Mwanza alipewa mkataba wa kujenga vyoo 12 wenye gharama ya bilioni 2.2.
Mgwatu amesema mkataba huo wa Mkandarasi wa GOPA Contractors Tanzania Limited ya Dar es Salaam
ulianza Januari 2021 na ulitegemea kukamilika Januari 2022,lakini kutokana na sababu mbalimbali wamemuongezea mkataba wa mwezi mmoja,hivyo wanategemea akamilishe Machi mwaka huu.
“Kwa ujumla maendeleo ya utekelezaji mradi huo siyo mazuri yupo nyuma,amekamilisha asilimia 65 tu ya kazi zake zote za mkataba,tumemuongezea mpaka mwezi Machi tunategemea atakuwa amekamilisha ujenzi wa vyoo hivi ili viweze kutumiwa na wanafunzi wanaotarajiwa,”amesema Mgwatu.
Amesema, maelekezo ya Mkuu wa Wilaya wameyapokea,sababu watakaa na menejimenti ya MWAUWASA lakini pia na wataalamu wa manunuzi waone ni njia gani sahihi za kimkataba za kuweza kufuata ili waweze kusitisha mkataba.
“Kwa sababu usipokaa vizuri unaweza kusitisha mkataba akienda mahakamani akakushinda,ndio maana nasema tutakaa na mwanasheria wa mamlaka na watu wa manunuzi,tutakaa na menejimenti na tutaipelekea bodi pia,tuone namna gani tunaweza kusitisha mkataba vizuri ili ata akienda mahakamani asiweze kutushinda,” amesema na kuongeza kuwa
“Sababu hii miradi ina fadhiliwa na shirika la Maendeleo ya Ufaransa na Benki ya uwekezaji ya Ulaya,nao
wanasehemu yao ya kuwataarifu,hivyo tutawapa taarifa na wao watatushauri njia gani tufuate za manunuzi ili tuweze kusitisha mkataba,”amesema Mgwatu.
Naye Mkandarasi wa kampuni ya GOPA Contractors Tanzania Limited ya Dar es Salaam ambayo inatekeleza mradi wa ujenzi wa vyoo 20 kwa shule 11 wilayani Nyamagana zikiwemo shule za msingi Nyakabungo na Sahara, Mhandisi Nelson Mdeka, amesema mradi umefikia asilimia 65.
Amesema walishinda kukamilisha ndani ya muda kutokana na baadhi ya changamoto zilitokea hivyo ameisha omba kuongeza muda (extension)ambayo wanaruhusiwa kimkataba ambapo wanaweza kukamilisha kwa muda ambao wameongezewa.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba