April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Gwajima ataka afua madhubuti za MTAKUWWA ili kuleta matokeo chanya katika kudhibiti vitendo vya ukatili hususan wa watoto

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Gwajima amezitaka Kamati zinazotekeleza Mpango wa Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kuweka mipango madhubuti ya kutokomeza ukatili hususan dhidi ya watoto huku akiwataka wajumbe wa kamati hiyo kwa mkoa wa Dodoma kuwa mfano na mikoa mingine ikajifunze kwao.

Hayo yamesema na Waziri Dkt.Gwajima wakati akifungua kikao kazi cha MTAKUWWA mkoa wa Dodoma huku akisema ukatili hususan wa watoto unapaswa kupunguzwa zaidi kama siyo kumalizwa kabisa.

Dkt.Gwajima amesema licha ya mafanikio mengi yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa kamati hizo lakini bado matukio ya ukatili ya wanawake na watoto ni mengi hivyo kamati zinapaswa kuongeza nmguvu zaidi katika afua za MTAKUWWA ili kuleta tija.

“Pamoja na jitihada zote zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau bado matukio ya vitendo vya ukatili yameendelea kujitokeza katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma ambapo, kati ya changamoto zinazoathiri jitihada za utekelezaji wa MTAKUWWA ni pamoja na utendaji usioridhisha wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto hususan kwenye ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa/vijiji,

“Utengaji na utolewaji duni wa fedha za utekelezaji wa afua za MTAKUWWA katika ngazi zote,ushirikiano mdogo wa kiushahidi kutoka kwa waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya watuhumiwa hususan watu au ndugu wa karibu na hivyo kusababisha kesi nyingi kushindwa kutolewa maamuzi na watuhumiwa kuachiwa huru na upungufu wa watendaji wa kada mbalimbali zinazohusika moja kwa moja katika kushughulikia masuala ya ukatili nchini kama vile Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Polisi na Wanasheria hususan katika ngazi za kata na vijiji/mitaa. “

Aidha amesema,uwepo wa mila na desturi zenye madhara ndani ya jamii zetu zikiwemo za ukeketaji na ndoa za utotoni ambazo zimeendelea kumkosesha haki za mtoto wa kike na kuathiri maendeleo na ustawi wake.

“Wote tunatambua madhara ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa Taifa ikiwemo ya kiuchumi, kiafya na kijamii na kuwa, ukatili huu unabaki kuwa changamoto kubwa na kizuizi cha jitihada za kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.”

Vilevile Dkt.Gwajima amesema  ukatili kwa watoto hususan unaofanywa na watu au ndugu wa karibu umekuwa na athari mbaya zaidi kwa ustawi na maendeleo ya watoto nchini huku akisema utatuzi wa changamoto za ukatili unahitaji sana jitihada endelevu za pamoja baina ya Serikali na Wadau.

Pamoja na mambo mengine Dkt.Gwajima ameitaka Kamati hiyo kuandaa mikakati madhubuti iliyoboreshwa itakayosaidia kuimarisha utendaji wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto ikiwemo kukamilisha uundwaji wa Kamati hizo na kuzijengea uwezo ili zitekeleze majukumu yao ipasavyo kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili.

Pia ameitaka kamati hiyo kuhakikisha rasilimali fedha zinatengwa na kutolewa kwa ajili ya utekelezaji wa afua za MTAKUWWA kama inavyoelekezwa katika Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali unaotolewa kila mwaka na Wizara ya Fedha na Mipango

Kwa mujibu wa Wziri huyo Wizara itaendelea kuratibu wadau wote ili kuongeza nguvu katika kujenga uwezo na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikakati mtakayokuwa mmeweka kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa vishiria vya ufanisi (scorecard) ili hatimaye kujilinganisha na maeneo mengine nchini.

Kwa upande wake  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amezitaka Kamati kuanzia ngazi ya Taifa kuufanya mpango kazi huo wa Taifa uonyeshe matokeo chanya kama ilivyotarajiwa.

Naye Mratibu wa mpango huo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Happiness Mugyabuso amesema katika utekelezaji wa mpango huo ulioanza mwaka 2017/2018 kumekuwa na changamoto nyingi katika jamii japokuwa kumekuwa na mafanikio kutokana na jithada zinazofanywa na Serikali na  wadau ikiwemo kuimarisha mifumo ya kitaasisi.

Awali mwakilishi wa  Mkuu wa Mkoa Dodoma Bernard Abraham amesema kuwa, chanzo kikubwa cha ukatili katika jamii ni uchumi wa kaya kuwa mdogo huku akisema utekelezaji wa mpango huo, nguvu kubwa ielekezwe katika kuimarisha  uchumi wa kaya.

“Sisi sote ni mashahidi tumekuwa tukishuhudia mtoto akichomwa moto kwenye vidole vya mikono yake kwa sababu tu amekula mboga,hii inamaanisha uchumi wa kaya bado ni mdogo,kwa hiyo tukilenga kwenye kuimarisha uchumi wa kaya pia kwa kiasi fulani inaweza kupunguza matukio haya  ya ukatili hususan wa watoto.