December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watakiwa kutumia Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kutatua changamoto

Na Cresensia Kapinga, TimesMajira,Online,Songea

WAKAZI wa Mkoa wa Ruvuma wametakiwa kutumia wiki ya sheria kwa kwenda kupata elimu juu changamoto mbalimbali ambazo wamekuwa wakikutana nazo ndani jamii ili waweze kujenga uelewa pindi wanapokutana na mashauri.

Mwito huo ulitolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Sekela Moshi wakati akitoa hotuba ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria inayofanyika katika viwanja vya Soko Kuu la Songea mjini, ambayo yalianza Januari 23 mwaka huu na kilele chake kikitarajiwa kuwa Februari mosi.

Maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kauli mbiu ya Zama za Mapinduzi ya nne ya Viwanda ,Safari ya Maboresho Kuelekea Mahakama Mtandao.

Jaji Moshi azungumza mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo,Dkt Julius Ningu ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bregedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge, alisema kuwa ni ukweli usiyopingika wananchi wengi wamekuwa hawazitambui kazi zinazofanywa na mahakama pindi wanapohitaji msaada wa kisheria ,hivyo wanatakiwa kutumia wiki hiyo kikamilifu kwa kujipatia elimu.

Alisema kuwa mahakama zimejipanga vema kuendelea kuboresha namna ya usikilizaji wa madai kwa kutumia mifumo mbalimbali ikiwemo ya kisasa (TEHAMA) ambayo itawafanya wananchi wazidi kuwa na uelewa pindi wanapotumia mitandao ya kiteknolojia namna ya kupata haki za madai yao .

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Sekela Moshi akisoma taarifa ya uzinduzi ya uzinduzi ya wiki ya sheria kwa wananchi na watumishi Mahakakama juzi iliyofanyika kwenye viwanja vya Soko kuu Manispaa ya Songea. (Cresensia Kapinga)

Mosha alisema kuwa katika wiki ya sheria Mahakama imewahusisha wadau mbalimbali katika mfumo wa utoaji wa haki kama vile Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ,Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ,Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ,Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Taasisi zinazotoa Msaada wa Kisheria (Legal Aid) Magereza,Takukuru na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS)ambazo hujumuika pamoja kutoa elimu na ushauri wa kisheria kwa wananchi bila malipo.

Kwa upande wake Katibu wa TLS Mkoa wa Ruvuma, Naomi John alisema kuwa Chama hicho kimekuwa kikitoa ushauri wa kisheria kwa wale wasio na uwezo baada ya kuwafanyia tathimini pamoja nakutoa elimu kupitia vyombo vya habari.

Naye Wakili wa Serikali katika taasisi ya Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) Abely Ngilangwa alisema kuwa kazi kubwa ya wakili wa Serikali ni kuishauri Serikali pale panapokuwa na mashauri yanayoihusu Serikali ili kuifanya iwe kwenye msimamo sahihi isiweze kuingia kwenye migogoro ambayo inaweza kuepukika .

Ngilangwa alisema kuwa hakuna mashauri (Kesi) ambazo mawakili wa Serikali watasema wameshindwa bali ni namna ya kujipanga jinsi ya kuweza kuishauri Serikali kwa kuwa masahuri yanakuwa na mambo mengi ambayo yanatakiwa kuwa na umakini.

Kwa upande wake mgeni rasmi Dkt. Ningu aliipongeza Mahakama jinsi wanavyoendelea kuboresha namna ya utoaji huduma kwa wananchi jambo ambalo litawasaidia wananchi kupatiwa huduma kwa wakati.

Dkt Ningu alisema kuwa Mahakana zimepunguza malalamiko mengi kwa Wananchi na kufanya waendelee kuwa na imani na mahakama zao.

Katika hatua nyingine Dkt Ningu aliipongeza mahakama ya mkoa wa Ruvuma kwa ujenzi wa vituo vya jumuishi vya utoaji haki na ukarabati wa majengo yake ili kuendana na mapinduzi ya nne ya viwanda ,matumizi ya tehema katika shughuli zake zote za utoaji haki,usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya video.