November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndalichako ataka TET kukamilisha uandishi vitabu 69 vya kiada

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amelitaka Baraza jipya la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET)kuhakikisha zoezi la kukamilisha uandishi wa vitabu 69 vya kiada vya sekondari linakamilika kabla ya mwaka 2022 kuisha. Ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza la Saba la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ambapo amesema zoezi hilo limechukua takriban miaka mitano likiwa linasuasua na hivyo kuiletea lawama Serikali.
“Nataka kuona vitabu vyote vya sekondari vikiwa vimekamilika kabla ya mwaka 2022 kuisha. Wakurugenzi watakaoshindwa kusimamia zoezi hili muwachukulie hatua stahiki kwa kuwa wapo chini yenu,” amesema Waziri Ndalichako.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameeleza kutoridhishwa kwake na mwenendo wa upokeaji maoni ya uboreshwaji mitaala ambapo amesema mchakato huo umetumia muda mrefu na kutaka Baraza hilo kuhakikisha zoezi hilo linakamilika mara moja.
“Mwanzoni zoezi la kupokea maoni mlikuwa mnalifanya kwa uwazi, tumewaona kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii lakini sasaivi mmekuwa kimya, sijui mnapokea maoni kisirisiri? Tokeni wazi Watanzania waone na wajue kazi hii muhimu mnaifanyaje. Inaleta mashaka kama kweli kazi hii tunaipa uzito unaostahili,” ameongeza Waziri Ndalichako.
Naye Mwenyekiti wa Baraza hilo, Profesa Maulid Mwatawala amemuahidi Mhe. Waziri Ndalichako kutekeleza kwa umakini na weledi mkubwa maelekezo yote aliyotoa ikiwemo kufanya mapitio ya mitaala na kuhakikisha malengo ya taasisi yanafikiwa na kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Awali akiongea katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema katika mwaka wa fedha 2021/22 pamoja na majukumu mengine TET imejikita katika kufanya mapitio ya mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu ili kuhakikisha kuwa inapatikana mitaala inayolenga kuwawezesha wahitimu kuwa na ujuzi wa kujiajiri, kuajiriwa na kumudu maisha ya kila siku.
Amesema kazi nyingine ni kukamilisha uandishi wa vitabu vya Sekondari vya masomo mbalimbali ikiwemo vya Sanaa, Sayansi na Ufundi ambavyo jumla yake ni 69.
Hafla hiyo ya uzinduzi ilikamilika kwa Wajumbe wote wa Baraza kukabidhiwa vishkwambi ambavyo watavitumia kama vitendea kazi ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao. Vishwambi hivyo vimepakiwa Sheria ya TET ya mwaka 2002, Hati idhini ya Baraza la TET, Waraka wa Elimu Na. 4 wa mwaka 2014, kiunzi cha Taifa cha mitaala kwa elimumsingi na ualimu na miongozo mbalimbali.