November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tamatamah:Kiwango cha uzalishaji mazao ya mifugo,uvuvi kimeongezeka

Na Omary Mtamike,TimesMajira Online,Kilimanjaro

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah imesema kuwa kiwango cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi na matumizi yake kimeongezeka ukilinganisha na kile kilichokuwepo mwaka 2020.

Dkt. Tamatamah ameyasema hayo jana wakati akisoma taarifa ya Wizara hiyo kwenye sherehe za ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambazo kitaifa zimefanyika mkoani Kilimanjaro kwenye Uwanja wa shule ya Msingi Nelson Mandela uliopo eneo la Pasua Manispaa ya Moshi.

“Kiwango cha uzalishaji wa samaki kupitia maji ya asili kwa mwaka 2021 kimefikia takribani tani 372,000 huku uzalishaji wa mazao hayo kwa tasnia ya ufugaji wag samaki ukifikia takribani tani 20,355 na wastani wa kiwango cha ulaji wa samaki hao kimeongezeka kutoka kilo 8.2 hadi kilo 8.5 kwa mtu kwa mwaka ” amesema Dkt. Tamatamah.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko (Wizara ya Mifugo na Uvuvi), Stephen Michael (kulia) akimfafanulia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah kuhusu kuongezeka kwa uzalishaji wa Nyama na Maziwa muda mfupi baada ya Dkt. tamatamah kufika kwenye banda la Kampuni ya Ranchi ya taifa (NARCO) jana ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kwenye uwanja wa Nelson Mandela, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Katikati yao ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. angelo Mwilawa.

Akizungumzia kwa upande wa sekta ya Mifugo, Dkt. Tamatamah amesema kuwa kiwango cha uzalishaji wa nyama kimeongezeka hadi tani 738,166 ukilinganisha na tani 701679 zilizozalishwa mwaka uliopita na kiwango cha uzalishaji wa maziwa kimefikia lita bilioni 3.4 ikilinganishwa na lita bilioni 3.1 zilizozalishwa mwaka uliopita.

Dkt. Tamatamah amebainisha kuwa kuongezeka kwa kiwango hicho cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi kumetokana na dhamira ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na uhaba wa chakula na lishe bora hapa nchini.

“Aidha maadhimisho haya ya Siku ya Chakula nchini huwa ni moja ya chachu za kuongeza uzalishaji wa mazao haya ya mifugo na uvuvi kwa sababu hutukumbusha kuwatendea haki wananchi kwa kuhakikisha chakula cha kutosha na chenye ubora kinapatikana na kinalindwa ili kisiharibike kabla au baada ya kuvunwa ili kimfikie mlaji kikiwa salama” Ameongeza Dkt. Tamatamah.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai ukubwa wa samaki wanaoweza kupatikana endapo vitendo vya uvuvi haramu vitadhibitiwa muda mfupi baada ya Kagaigai kufika kwenye banda la maonesho la Mifugo na Uvuvi jana ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kwenye uwanja wa Nelson Mandela, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo Dkt. Tamatamah amewasihi wananchi kuendelea kutumia vyakula vinavyotokana na mazao ya mifugo na Uvuvi kwa wingi ili kufikia viwango vilivyowekwa na Shirika la Umoja wa mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) ambalo husisitiza kila mtu kula wastani wa kilo 20.3 za samaki, kilo 50 za nyama na lita 200 za maziwa kwa mwaka.

Maadhimisho ya Siku ya chakula Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kumkumbusha mwananchi kuzingatia lishe bora wakati wote ili kuondokana na changamoto ya tatizo la udumavu na kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora wakati wote.