November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCCIA kushiriki kongamano la Baraza la Biashara la Afrika

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online,Dar

CHEMBA ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) itashiriki katika kongamano la siku tatu la Baraza la Biashara la Afrika litakalofanyika kuanzia Novemba 10, Jijini Cairo, Misri.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Judith Karangi, Jijini jana.

Karangi amesema Chemba ya Tanzania imealikwa kuhudhuria kongamano hilo na kwamba imepokea fomu za utambulisho wa bidhaa zinazopatikana nchini na kwamba tayari fomu hizo zimesambawa nchini ili zijazwe na wazalishaji wanachama wa chemba na wazalishalji wengine.

“Fomu za utambulisho wa bidhaa zinapatikana katika ofisi za TCCIA nchini kote na tumepanga kuzitoa kwenye taasisi nyingine ili upatiakanaji wake uwe rahisi,” amesema Karangi na kuwaomba wazalishaji na hasa wanachama wa TCCIA kujaza fomu hizo ili hatua zinazofuata zitekelezwe wakati muafaka.

“Kongamano hili ni fursa kwa sekta binafsi nchini katika kubaini soko liliyomo Afrika na namna ya kuingiza bidhaa za Tanzania kwenye orodha ya bidhaa zilizozalishwa Afrika.

Hii ni ni sehemu ya jitihada pana ya kimkakati ya kuzifanya bidhaa za Afrika kushindana katika soko la Afrika na masoko mengine ya kimataifa,” amefafanua.

Amehimiza wanachama wa TCCIA na sekta binafsi kwa jumla kuchangamkia fursa hii na kusisitiza kwamba ushiriki wa sekta binafsi katika kongamano hilo ni muhimu kwani ni fursa itakayosaidia kukuza na kuboresha biashara na kuifanya Tanzania inufaike kwa kuwemo katika umoja huo. Aidha kongamano hilo litaiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia, ameeleza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya wafanyabiashara, viwanda na Kilimo (TCCIA), Judith Karangi, akizungumza na waandishi wa habari juu ya ushiriki wao katika kongamano lililoandaliwa na Baraza la Biashara Afrika litakalofanyika Cairo Nchini Misri kuanzia Novemba 10 hadi 12, mwaka na kuwataka wadau kujitokeza kushiriki katika kongamano hilo.

Aidha, Karangi amemshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kufanikisha kongamano la uwekezaji lililofanyika Dodoma tarehe 4 Oktoba, na kusisitiza baada ya mkutano huo ushiriki wa sekta binafsi katika kongamano la Cairo ni wa wazi na umuhimu wake ni dhahiri pia.

“TCCIA itaendelea kushirikiana na wadau wengine kutoka sekta binafsi kutoa elimu kwa wanachama wetu ili waweze kupata uelewa zaidi juu ya muhimu wa soko la pamoja la Afrika na itakavyoweza kuwainua katika mauzo na kukuza vipato vyao,” ameahidi Bi.Karangi

Mkurugenzi Mtendaji huyo ametoa wito kwa wazalishaji na wajasiriamali ambao hawajajisajiri na TCCIA wafanye hivyo ili wanufaike na fursa zipatikanazo chini ya mwamvuli wa chemba hiyo ambayo ni kiunganishi cha masoko ya bidhaa zao na taratibu nyingine.

“TCCIA ina wataalumu wabobezi katika nyanja mbalimbali hivyo wajiunge nasi ili wapatiwe huduma nzuri zitakazowanyanyua kutoka hatua moja kibiashara na kwenda hatua nyingine na kuwafanya wajivunie kuwa wanachama wa Chemba hii,” amesema Karangi.

Kongamano hilo litafanyika kuanzia Novemba 10 hadi 12 mwaka huu na inatarajiwa wadau wa sekta binafsi wa nchi za Afrika watashiriki kongamano hilo ambalo linajulikana kama Africa Union Private Sector Forum.