November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIC latoa msaada vifaa vya usalama barabarani Shinyanga

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga

SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) mkoani Shinyanga limetoa vikoti vinavyoakisi mwanga na vibao vya kuongozea magari kwa shule za msingi zilizopo kandokando ya barabara kuu ili kuwasaidia wanafunzi kuvuka barabara kwa usalama.

Meneja wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) mkoani Shinyanga Hamis Mohamed (kushoto) akimkabidhi Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Joseph Paulo moja ya vibao vitakavyowasaidia wanafunzi wa shule za msingi mjini Shinyanga kuvuka kwa usalama kwenye vivuko vilivyopo  barabarani jirani na shule zao kulia ni Kamanda wa Usalama barabarani mkoa, Emmanuel Kilakala (Picha zot na Suleiman Abeid)

Akikabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tano Meneja wa Shirika la Bima la Taifa mkoani Shinyanga Hamis Mohamed amesema lengo la msaada huo ni kuwasaidia wanafunzi kuweza kuvuka barabara kwa usalama na kuepusha kugongwa na magari.

Mohamed amesema mara nyingi wanafunzi wengi hukutana na changamoto pale wanapokuwa wanavuka vivuko vya barabarani pamoja na kwamba kuna alama zinazowataka madereva kusimama pindi watembea kwa miguu wanapovuka barabara.

Amesema pamoja na kuwepo alama hizo baadhi ya madereva hawana tabia ya kutii sheria za usalama barabarani na badala yake huweza kusababisha ajali kwa kuwagonga watembea kwa miguu pale wanapovuka barabara hasa wanafunzi wadogo wa shule za msingi.

Kamanda wa Usalama barabarani wilayani Shinyanga, Emmanuel Palangyo (kulia) Meneja wa Shirika la Bima la Taifa mkoani Shinyanga, Hamis Mohamed (mwenye T-shirt nyeupe), Mwenyekiti Kamati ya Usalama barabarani Wilson Majiji (katikati) na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP, Joseph Paulo wakiangalia refractor zilizotolewa na Shirika la Bima

“Hawa vijana wetu mara nyingi hukumbana na changamoto pale wanapovuka kwenye vivuko vilivyopo barabarani, kama alivyoeleza hapa Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabara ya mkoa kwamba si watu wote wanaotii sheria,”

“Wapo baadhi ya madereva ni wakaidi pamoja na kwamba kuna alama lakini hawazifuati, hivyo sisi kama Shirika tumeamua kuwaunga mkono wenzetu wa Polisi wa Usalama barabarani kwa kuwapatia vibao pamoja na refractor jacket ili pindi wanapovuka barabara wavitumie kusimamisha magari wavuke kwa usalama,” ameeleza Mohamed.

Amefafanua kuwa vibao na refractor jacket vitasambazwa katika shule zote za msingi zilizopo kandokando ya barabara kuu ambako mara nyingi ndiko kuna matukio ya ajali za mara kwa mara zikuhusisha pia kugongwa kwa wanafunzi pindi wanapovuka barabara hizo.

Sehemu ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwenge iliyopo mjini Shinyanga wakiwa na vifaa vya kuwasaidia kuvuka barabara kwa usalama vilivyokabidhiwa na Shirika la Bima la Taifa mkoani Shinyanga, kutoka kushoto ni mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Mwenge, Mika Paulo na Kamanda wa Usalama barabarani wilaya ya Shinyanga, Emmanuel Palangyo

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani mkoani Shinyanga, Wilson Majiji amelishukuru Shirika la Bima la Taifa kwa msaada huo ambapo alisema mbali ya kuwasaidia wanafunzi kuweza kuvuka barabara kwa usalama lakini itakuwa ni sehemu ya elimu kwao juu ya matumizi salama ya barabara.

“Naomba nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Shirika hili ambalo limetuwezesha kupata vifaa hivi ambavyo kwa kweli vitakuwa sehemu ya elimu ya usalama barabarani kwa watoto wetu, japokuwa kwa sasa hapa mkoani kwetu ajali kwa sasa zimepungua kwa kiasi fulani,” ameeleza Majiji.

Majiji amesema ni muhimu kwa wahusika kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba suala la elimu ya matumizi sahihi ya barabara linapaswa kutolewa kwa jamii mara kwa mara ili kuhakikisha hapatokei ajali zinazoweza kusababisha watu kupoteza maisha.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mwenge iliyopo mjini Shinyanga, Mika Paulo amelishukuru Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga pamoja na Shirika la Bima la Taifa kwa msaada wa vifaa hivyo ambavyo kwa kiasi kikubwa vitawasaidia wanafunzi kuweza kuvuka kwa usalama kwenye kivuko cha barabara kilichopo jirani na shule yao.

Kamanda wa Usalama barabarani wilayani Shinyanga, Emmanuel Palangyo akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya msingi Mwenge mjini Shinyanga ya jinsi ya kutumia vibao vya kusimamisha magari ili waweze kuvuka barabara kwa usalama ambapo watakuwa wakifanya zoezi hilo asubuhi wanapokwenda shule na jioni wanapotoka shule.

“Tunashukuru sana kwa msaada huu ambao ni utakuwa ni sehemu ya ulinzi kwa watoto wetu, hata hivyo tunawashukuru askari wetu wa usalama barabarani ambao mara nyingi nyakati za asubuhi na jioni hukaa eneo la kivuko cha barabara ili kuhakikisha watoto wanavuka salama,”

Paulo amesema kutokana na msaada huo wanafunzi wa shule ya msingi Mwenge mara nyingi huwa na changamoto ya kuvuka barabara kwa usalama nyakati za asubuhi wanapokwenda shuleni na jioni wanapotoka shule na kwamba vifaa hivyo vitakuwa ni sehemu ya elimu kwao ya jinsi ya matumizi salama ya barabara.

Awali Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani Shinyanga, Emmanuel Kilakala na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Joseph Paulo walipata fursa ya kutoa shukrani zao kwa Shirika la Bima la Taifa mkoani Shinyanga kutokana na msaada huo.

“Nichukue fursa hii kutoa shukrani zetu za dhati kwa Shirika letu la Bima ya Taifa kwa msaada walioutoa ukiwa na lengo la kuwasaidi wanafunzi wetu kuvuka kwa usalama kwenye vivuko viliyopo barabarani maeneo ya shule zao,”

“Ukweli ni kwamba msaada huo utatusaidia sana kudhibiti ajali ambapo pale zinapotokea huwa na madhara makubwa, vibao na refractor mlivyovitoa vitasaidia sana kuzuia ajali katika maeneo ya shule zetu zilizopo pembezoni mwa barabara kuu, lakini pia vitakuwa ni sehemu ya elimu kwa watu wengine,” alieleza Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, ACP Joseph Paulo.