November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Nimeridhishwa na ujenzi wa bandari ya Karema

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Katavi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa bandari ya Karema na kusema kwamba ameridhishwa na ubora na hatua iliyofikiwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Bandari ya Karema wilayani Tanganyika mkoa wa katavi, Agosti 25, 2021.  Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Eric Hamissi. Bandari hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwakani.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Ameyasema hayo jana baada ya kukagua mradi huo unaojengwa katika kata ya Karema wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.

Waziri Mkuu amesema Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kwa dhati kuhakikisha miradi yote inayoendelea na mingine inayo anza inakamilika kwa wakati.

Amesema mradi huo ambao utakuwa ni kiunganishi cha usafirishaji wa mizigo na abiria katika bandari hiyo na bandari ya Karemie iliyoko Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Nimefurahi kusikia mradi huu umefikia asilimia 50 na ifikapo Machi mwakani utakuwa umekamilika na tayari kwa matumizi, hivyo nawaomba wananchi mchangamkie fursa ya uwepo wa mradi huu.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Bandari ya Karema wilayani Tanganyika mkoa wa Katavi, Agosti 25, 2021.  Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Eric Hamissi na wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwananvua Mrindoko. Bandari hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi machi mwakani.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Erick Hamiss amesema ujenzi wa mradi wa bandari ya Karema umefikia asilimia 50 ya utekelezaji.

Amesema ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 47.97 ulianza Agosti, 2019 na unatarajiwa kukamilika Machi, 2022. Mradi huo umeajiri watu 300 kati yake raia wa kigeni ni tisa tu.

“Mradi huu ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi nchini hususan katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Tanganyika na nchi jirani za Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.”

Bandari ya Karema wilayani Tanganyika mkoa wa Katavi ambayo Ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwakani. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Agosti 25, 2021 alikagua ujenzi wa Bandari hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema mkoa umejipanga kuzitumia vizuri fursa zitokanazo na ujenzi wa mradi huo kwa ajili ya kukuza uchumi.