Na Joyce Kasiki, TimesMajira,OnlineKagera
UJENZI wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera (Kagera RVTSC) kinachojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya China unatarajia kukamilika Novemba 27, mwaka huu . Chuo hicho kinatarajiwa kudahili wanafunzi 1,400.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga katika ziara yake mkoani humo ili kuona maendeleo ya mradi huo, ambapo ameridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa pamoja na kiwango cha ujenzi.
Amesema chuo hicho kikikamilika kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kudahili jumla ya wanafunzi 400 wa kozi ndefu na wanafunzi 1,000 wa kozi fupi na kwamba kitaweza kutoa huduma ya malazi kwa wanafunzi 360.
Kipanga amesema Serikali pia inajenga vyuo vya aina hiyo katika mikoa ya Rukwa, Njombe, Geita na inakusudia kujenga katika mkoa wa Simiyu. Lengo ni kuhakikisha kila mkoa unakuwa na chuo kikubwa cha umahiri ambacho kitatoa mafunzo ya kozi maalum kulingana na mazingira na shughuli za kiuchumi za Mkoa husika.
“Mfano hapa Kagera kuna ziwa kwa hiyo tunatarajia chuo hiki pamoja na kozi nyingine, kitoe kozi za uvuvi na kilimo kwa kuwa hapa mnalima kahawa, migomba na mazao mengineyo,” amesisitiza Kipanga.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo, ununuzi wa mitambo na zana za kufundishia na kujifunzia pamoja na uwekaji wa samani.
Amesema mradi unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya sh. bilioni 22 na kwamba kwa ujumla mpaka sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 80.
Naye Meneja Msaidizi wa kampuni ya Shanxi Construction Investment Group ya China ambayo ndiyo inayotekeleza ujenzi wa mradi huo, He Tianan alishukuru kutembelewa na kiongozi huyo na ameahidi kukamilisha ujenzi kwa wakati uliopangwa.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba