Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Mafia
WAZIRI wa Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,William Lukuvi ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kuchangamkia fursa ya uwekezaji kwani Mafia ni kisiwa chenye fukwe nzuri inayohitaji wawekezaji wakubwa katika sekta ya utalii .
Lukuvi ameyaeleza hayo katika kijiji cha Gonga ,wakati wa ziara yake ya kutatua kero za ardhi kwenye wilaya mbalimbali mkoani Pwani ,akitangaza Kampeni maalum “TOKOMEZA KERO ” ambapo alipata fursa ya kujionea fukwe za bahari ambazo hazina mkakati mahsusi wa kuvutia wawekezaji wakubwa kwenye sekta ya utalii .
“Nasisitiza hakuna budi mkachangamkia fursa hii na mhakikishe mnaifanyia kazi kwa maslahi ya wilaya ,mkoa na Taifa kuongeza pato na kuinua uchumi ”
“Sikutarajia kukuta vivutio vizuri hivi wilayani hapa ,hasa katika upande wa fukwe ambazo zimeambaa eneo kubwa la kisiwa pamoja na ardhi ambayo ni kubwa na ikipangwa kimkakati itakaribisha wawekezaji wengi kuwekeza kisiwa hiki tulivu “amefafanua Lukuvi .
Pia amekagua mashamba makubwa yanayolalamikiwa katika kijiji cha Gonga kwenye mashamba ya Utumaini ekari 4,040 na Kigomani ekari 670 ambayo mmiliki wake yuko hatua za kupata wabia wa kuwekeza .
Lukuvi baada ya kusikiliza pande zote zinazohusika na mgogoro huo akaelekeza halmashauri kupitia nyaraka za umiliki wa maeneo hayo kwa umakini kabla ya kumshauri hatua za kuchukua .
Mkuu wa Wilaya ya Mafia ,mhandisi Martin Ntemo amesema kumekuwa na migogoro ya muda mrefu ya ardhi iliyohusu zaidi maeneo makubwa yanayomilikiwa na watu ama kampuni binafsi yakiwa katika mgogoro na wananchi wanaoishi katika vijiji jirani na maeneo hayo .
Kisiwa cha Mafia ni kisiwa cha tatu kwa ukubwa nchini kikiunda moja ya wilaya saba za mkoa ,kina ukubwa wa kilometa za mraba 972 ambazo kati yake kilometa za mraba 407 ni nchi kavu na kilometa za mraba 565 ni enei la maji ,kuna wakazi 53,083 ambao wanajishughulisha na shughuli za utalii .
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea