MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt.Tedros Ghebreyesus ametaja mambo matano muhimu ya kila mtu kuzingatia katika kipindi hiki cha janga la virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.
Mambo hayo ni kuzingatia ulaji wa vyakula bora, vyenye lishe itakayofanya kinga ya mwili kuimarika, kupunguza unywaji wa pombe pamoja na vinywaji vyenye sukari.
Jambo la tatu alisisitiza jamii kuacha kabisa uvutaji wa sigara, kufanya mazoezi na kujiweka vyema kiakili na kisaikolojia ili kuepuka msongo wa mawazo na sonona.
Katika makala haya, Mwandishi Wetu anazingatia hoja namba tatu ya kutovuta sigara.
Taarifa ya WHO kuhusu COVID-19 inasema wavutaji wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata korona kali kuliko wasiovuta.
WHO pia inasisitiza kuwa, wavutaji wanaweza kuwa na ugonjwa wa mapafu tayari au upungufu wa nguvu kwa kiungo hicho muhimu kinachomsaidia mtu kupumua kitu kinachoweza kuongeza ukali wa ugonjwa.
Taarifa hiyo inaungwa mkono na Shirika la Kimataifa Dhidi ya Kifua Kikuu na Magonjwa ya Mapafu kwamba uvutaji tumbaku hudhoofisha mfumo wa kinga mwilini na hivyo kuufanya ushindwe kudhibiti vizuri maambukizi.
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Uhusiano wa Magonjwa ya Moyo na Tumbaku nchini Marekani, Dkt Jonathan Winickoff anasema mapafu ya wavutaji wengi wa sigara yanakuwa dhaifu kutokana na athari za moshi wa sigara.
Kwa sababu hiyo anasema mvutaji anapoambukizwa COVID-19 inakuwa rahisi kuingia kwenye hatua mbaya ya kuhita msaada wa mashine za kupumua.
Utafiti uliohusisha zaidi ya wagonjwa 1,000 wa Korona na kuchapishwa kwenye jarida la Afya la New England Journal of Medicine toleo la mwezi Februari 2020, ulionyesha kuwa wavutaji wa zamani na wa sasa walishindwa kupona kirahisi.
Kilichotokea, anasema zaidi ya asilimia 25 ya wagonjwa waliohitaji vifaa maalum vya kupumulia na walilazwa vyumba vya wagonjwa mahutuhi (ICU) na wengi wao walifariki.
“Tumbaku pia ni sababishi kubwa la magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo saratani, magonjwa ya moyo, kisukari na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa. Watu wanaougua magonjwa yasiyoambukiza pia wako kwenye hatari kubwa ya kupata COVID-19,” anafafanua Dkt Winickoff.
Anasema wavutaji wengi wanapata taabu ya kuacha sigara lakini wakiwaona wataaalamu wa afya ni rahisi kupewa ushauri na usaidizi wa njia rahisi kuachana na tabia hiyo.
Jambo jingine kwa wavutaji, Dkt.Winickoff analitaja ni mvutaji kuwa rahisi kupeleka maambukizi mdomoni wakati wa uvutaji.
Wakati kitendo cha kuvuta humaanisha vidole, na hata sigara zenye maambukizi, kugusana na midomo.
Vilevile anasema kuvuta bidhaa kama shisha mara nyingi huhusisha kushirikiana vipande vya mdomoni na mirija, vitendo ambavyo huraisisha kuenea kwa virusi vya corona kwenye jamii na sehemu za starehe.
Je, ni hatua gani zichukuliwe?
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania, Lutgard Kagaruki anasema:“Ni wakati muafaka kwa Tanzania kupitisha sheria madhubuti ya kudhibiti matumizi ya tumbaku inayoendana na matakwa ya Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku wa WHO.
“Lengo ni kuwakinga wasiovuta dhidi ya moshi wa tumbaku na kuwasaidia wavutaji kuacha kwa kuzingatia athari za hatari kwenye afya ya mfumo wa hewa na janga la sasa la COVID-19.”
Anasema ni fursa kwa Tanzania kupitia upya sera zake za kudhibiti matumizi ya tumbaku kuhakikisha ulinzi imara wa wasiovuta dhidi ya moshi wa tumbaku na pia kuwasaidia wavutaji kuacha.
“Tanzania ilitunga Sheria ya Kudhibiti Bidhaa za Tumbaku 2003 ambayo lengo lake kuu ni kupunguza matumizi ya tumbaku na athari zake kwa kulinda watu walio chini ya miaka 18 na wengine wasiovuta dhidi ya ushawishi wa kutumia bidhaa za tumbaku,” anasema Kagaruki.
Zaidi ya hapo, anasema Tanzania iliridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO FCTC) mwaka 2007.
“Hata hivyo, sheria ya kudhibiti tumbaku (TPRA, 2003) ina mapungufu mengi na hivyo kushindwa kulinda umma wa Watanzania kwa uhakika dhidi ya majanga yanayoyasababishwa na tumbaku,” anasema Kagaruki.
Upungufu huo ndani ya sheria, anasemaumetoa mwanya kwa kampuni za tumbaku kuongeza matangazo, ufadhili na promosheni za bidhaa za tumbaku, ikiwemo kugawa sigara za bure hasa kwenye majengo ya starehe.
Tangu kuridhiwa kwa Mkataba wa FCTC mwaka 2007, Kagaruki anasema juhudi zimefanywa na wadau mbali mbali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha sheria mpya ya kudhibiti tumbaku inatungwa; bahati mbaya, hadi leo, zaidi ya miaka kumi, bado muswada wa sheria hiyo haujapelekwa bungeni.
Ndani ya Afrika Mashariki ikiwemo Zanzibar, nchi nyingi za Afrika na hata dunia kwa ujumla zimechukua hatua ni Tanzania pekee ambayo haina sheria madhubuti ya kudhibiti matumizi ya tumbaku.
“Ni wakati muafaka sasa, kwa Tanzania kutunga sheria madhubuti, kuukinga umma wa watanzania dhidi ya majanga yanayosababishwa na tumbaku hasa hasa COVID-19,” anasema Kagaruki.
More Stories
Hivi ndivyo TASAF ilivyoshiriki kumaliza kilio cha wananchi Kata Bwawani, Arusha
Mfumo unavyokwamisha wanawake kuwa viongozi
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni