November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makamu wa Pili wa Zanzibar kufunga Maonesho ya Sabasaba

Na Penina Malundo

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Abdullah anatarajia kuwa mgeni rasmi katika kufunga maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) na kutoa tuzo kwa washindi wa zoezi la ukaguzi wa banda bora kwenye maonesho hayo.

Maonesho hayo yalianza Juni 28 mwaka huu na kumalizika leo ambapo jumla ya wageni 121 ambao ni viongozi wa chama na serikali, mabalozi, wakuu wa taasisi za umma, binafsi, mashirika ya kimataifa na viongozi wa dini walihudhuria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika viwanja vya Sabasaba Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema kipindi cha maonesho, matukio kadhaa yenye kujenga kuongeza ufanisi katika sekta ya biashara yaliweza kufanyika, ikiwemo mikutano ya biashara kwa njia ya mtandao ambayo ilianza kufanyika tangu Juni 30 mwaka huu.

Alisema pia ndani ya maonesho hayo, kulifanyika uzinduzi wa tela la trekta lililotengenezwa na Kampuni ya Kilimanjaro Machine Tools (KMTC) iliyo chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), ili kutangaza teknolojia ya kilimo inayotengezwa nchini uliofanyika Julai 6 mwaka huu.

“Uzinduzi wa mfumo wa taarifa za biashara uliofanyika Julai 8 mwaka huu ambapo lengo la kuanzishwa kwake ni kujenga na kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara, kufahamu taratibu za kufanya biashara ya kimataifa,” alisema.

Alisema sambamba na maonesho hayo, pia utekelezaji wa miongoni na tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19, zinazotolewa na Wizara ya Afya zinatekelezwa ipasavyo kwa kushirikiana n Kamati Maalumu ya Kitaifa ya masuala ya afya wakati wote wa maonesho hayo.

“Kupitia miongozo hiyo, tumeweza kupunguza msongamano katika milango ya kuingilia kwa kuhamasisha watembeaji kukata tiketi kwa njia ya mtandao, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuweka vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali ya uwanja na uhamasishaji wa uvaaji wa barakoa,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jocate Mwegelo alisema tangu maonesho yalivyoanza hadi jana hakuna
matukio ya uvunjifu wa amani yoyote yaliyotokea.

“Tumemaliza shughuli hii salama, hatujapata changamoto pia ya masuala ya usalama barabarani, Jeshi la Polisi nalo limefanya kazi yake kubwa kwa kweli tunawashukuru wote waliofika katika maonesho haya, tuombe pia watu wajitokeze kwenye kufunga,” alisema.