Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online
ILI kusaidia wimbi la vijana kutojiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya Diwani wa Kata ya Majengo, Salim Perembo ameandaa ligi ya sodo ya Perembo Cup, lengo likiwa kuwaunganisha vijana pamoja.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa ligi hiyo, Diwani Perembo amesema kuwa, kilichomsukuma kuandaa ligi hiyo ni ahadi kwa kuwa wakati anaomba kura kwa wananchi suala la michezo ni jambo ambalo aliliahidi kulifanyia kazi.
Perembo amesema kuwa, kata hiyo ni moja kati ya kata ambazo vijana wengi wameathirika na matumizi ya madawa ya kulevya hivyo kabla hawajapambana na kutokomeza suala hilo lazima kwanza awakutanishe vijana pamoja.
“Ningeomba hata wenzetu wa madawa ya kulevya wajiunge pamoja, na vijana wenzao na kuwaeleza athari za madawa ya kulevya na namna zinavyopoteza nguvu kazi ya Taifa,”alisisitiza Diwani Perembo.
Diwani Perembo amesema kuwa, ukizungumzia maendeleo huwezi kuiacha sekta hiyo ya michezo kwani katika michezo hiyo lazima kila mmoja acheze kwa ufanisi zaidi ili kutoa wachezaji bora, kwani ametengeneza mazingira ya kutafuta vipaji kwenye maeneo yao lengo ni kukuza vipaji vyao pamoja na kuimarisha afya zao.
Lakini pia amesema kuwa, wakati wakiendelea na ligi hiyo ya sodo watafikia hatua ya kutengeneza robo fainali ambapo wataanzisha ligi ya gozi ambayo wataalika timu za nje kutoka kwenye kata zote 27 za Tanga jiji.
“Ligi yetu hii inashirikisha timu 14 ambazo zimepangwa katika makundi matatu ikiwemo kundi moja la timu 5 ambapo kila kundi lenye timu 5 tutatoa timu 3 kwa maana ya kwamba wa kwanza, wapili na tatu, “amesema Perembo.
Aliongeza kuwa katika kundi lenye timu lenye timu 4 litatoa timu 2 na baada ya hapo watacheza robo fainali ya Mkoani kisha watacheza nusu fainali.
Perembo alisema kuwa kuwa yapo maendeleo ya maeneo, watu, lakini pia na ulinzi wa wananchi ambapo katika maendeleo ya wananchi ni pamoja na michezo ambapo wamezingatia mambo mengi jambo kubwa ni kuwakusanya watu.
Diwani Perembo ameahidi kuwa kila mwaka atahakikisha ligi ya Perembo Cup inakuwepo ambapo kwa kipindi hiki wameanza na ligi ya mpira wa sodo huku baadaye wakihamia kwenye mpira wa gozi.
Awali akifungua ligi hiyo ya Perembo Cup Mstahiki Meya wa jiji la Tanga Abdulrahman Shiloo alimpongeza diwani huyo kwa kuamua kuandaa ligi hiyo huu akitaka madiwani wengine kuiga mfano wa diwani Perembo.
Meya Shiloo alisema kuwa michezo hiyo itasaidia kuimarisha afya za vijana wao lakini kubwa kuwafurahisha mashabiki na wakazi wa kata hiyo ya majengo na maeneo ya jirani.
Alisema ligi hiyo itasaidia kuimarisha umoja na mshikanano baina ya wakazi wa majengo pamoja na vijana hivyo amewasihi vijana hao kumuona mchezo huo wa sodo kama sehemu ya kujiendeleza.
“Msitumie fursa ya ligi hii kugombana, kuburuzana, kutukanana na kutengeneza, uhasama kwakuwa lengo letu sisi ni moja na kuwaonyesha watu wa Tanga na watu wa Majengo kuwa ni kitu kimoja, “alibainisha Meya Shiloo.
Ligi ya Perembo Cup inatarajiwa kudumu takribani mwezi mmoja, na nusu ambapo imenzaa tarehe 10 na kumalizika mwezi agosti mwishoni.
More Stories
Wafanyabiashara wakutana Dar,kujadili hali ya biashara
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo