Na Zena Mohamed,TimesMajira Online
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa maagizo 10 kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wakayasimamie na kuyafanyia kazi katika majukumu yao ya kikazi.
Pamoja na kuhakikisha wanapima maeneo yote ya taasisi za serikali ili waweze kupata hati miliki za maeneo hayo.
Majaliwa ametoa maagizo hayo leo jijini hapa wakati akifungua mafunzo kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi.
“Kuna mambo mahususi ambayo mtatakiwa kwenda kuyasimamia katika maeneo ya kazi ikiwemo suala la ulinzi na usalama, miradi ya maendeleo ambayo Serikali inatenga fedha nyingi kugharamia,”amesema.
Waziri Mkuu aliagiza kuwa, ”Kuboresha utawala bora ikiwemo matumizi mazuri ya sheria ya kumpumzisha mtu saa 48 ndani ambapo imeonekana viongozi wengi wamekuwa wakitumia vibaya sheria hiyo huku wakiwaumiza wananchi,”ameeleza.
Akizungumzia agizo la kutatua migogoro aliwataka wateule hao kusisimamia tija ya utendaji kazi wao ikiwemo kutumia njia bora za kutatua migogoro iliyopo miongoni mwa wananchi hasa wakulima na wafugaji.
Amesema, migogoro ambayo imekuwa ikidumu kwa muda mrefu katika maeneo yao ya kazi ni pamoja na migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji na mipaka.
“Mkatumie njia bora za kutatua migogoro mfano huko Njombe, Kiteto, Ruvuma kumekuwa na migogoro ambayo mkishirikiana na viongozi wenu wa chini mnaweza kuimaliza,”ameeleza.
Agizo la miradi ya maendeleo amewasisitiza wateule hao kuhakikisha fedha zinazotengwa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo zinasimamiwa na kutumika vizuri pasipo kuingiza vitendo ya ubadhirifu.
Amesema, wanatakiwa kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia mapato ya ndani inatekelezwa kwa ufasaha na kukamilika kwa wakati.
“Kuna miradi inayotekelezwa na Serikali Kuu nayo isiachwe hakikisheni inatekelezwa kwa sababu ninyi ndio wasimamizi wa shughuli zote za serikali katika ngazi ya mkoa,”ameeleza.
Katika agizo la utawala bora aliwasisitiza kusimamia utawala bora katika maeneo yao ya kazi ikiwemo kuongeza ushirikiano na viongozi kuanzia ngazi ya wilaya hadi kwenye kata.
Amesema, maendeleo yatapatikana endapo suala la utawala bora litaboreshwa.Alibainisha kuwa, kumekuwa na matumizi mabaya ya sheria ya kumpunzisha mtu saa 48 na kusisitiza sheria hii iangaliwe upya.
“Sheria hii imekuwa ikileta migogoro kati ya wananchi na serikali kwa sababu imekuwa ikitumiwa vibaya, yaani kila anayekosea mbele yako unataka awekwe ndani kinyume na sheria yenyewe inavyoelekeza,”ameeleza.
Kwenye elimu aliwataka wakuu wa mikoa na makatibu tawala kuimarisha mazingira ya kufundishia katika shule zote za sekondari na msingi.
“Mkafuatilie mwenendo mzima wa elimu katika maeneo yenu na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora ikiwa ni pamoja na kuweka mipango mikakati ya kuongeza ufaulu.
“Hakikisheni maeneo yote yanayomilikiwa na Serikali ikiwemo na taasisi zake zote maeneo yake yamepimwa na hati zake zipo,”ameeleza.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa, Ummy Mwalimu amewataka wateule hao kuyapa kipaumbele mambo matano katika mikoa yao.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni afya, elimu, barabara, ukuzaji wa uchumi na uendelezaji wa miji na vijiji.
“Nampongeza sana Rais Samia kwa kuwaamini ninyi miongoni mwa wengi hakuna shukurani nzuri ya kumpa zaidi ya kutekeleza kwa ufasaha yale ambayo ametutuma,”ameeleza.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi amesema, lengo la kutoa mafunzo hayo kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala ni kuwajengea uwezo binafsi.
Amesema, mafunzo hayo yatafanyika kwa siku nne ambapo kutakuwa na mada mbambali zinazohusu masuala ya uongozi bora.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi