November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KMC: Hatujakata tamaa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

UONGOZI wa klabu ya KMC umeweka wazi kuwa licha ya kutolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam ‘Azam Sports Federation Cup (ASFC)’ lakini hawatakata tamaa na sasa wanarudisha nguvu katika mechi zao zilizosalia za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL).

Katika mchezo huo wa FA, KMC ilikubali kichapo cha goli 2-0 kutoka kwa wenyeji Dodoma Jiji FC ambazo zilifungwa dakika ya 19 na Seif Karihe huku goli la pili katika mchezo huo likifungwa dakika ya 41 na Dickson Ambundo.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Christina Mwagala amesema kuwa licha ya wachezaji wao kuonesha kiwango bora na kutengeneza nafasi nyingi za magoli katika mchezo huo lakini  bahati haikuwa upande wao.

Amesema kuwa, kocha mkuu wa klabu hiyo John Simkoko pamoja na msaidizi wake Habib Kondo wameweka wazi kuwa, kutoleka katika michuano hiyo hakujawavunja nguvu kwani jambo kubwa kwa sasa ni kushinda mechi zao zilizosalia za Ligi Kuu.

Kazi kubwa iliyo mbele yao kwa sasa ni kufanyia kazi makosa waliyofanya kutolewa katika michuano hiyo ili kuweza kuendelea kufanya vizuri na kuhakikisha wanasalia katika nafasi tano za juu katika msimamo wa Ligi.

Katika mechi 27 walizocheza hadi sasa, KMC wapo nafasi ya tano wakiwa na pointi 40 walizopata baada ya kushinda mechi 11, sare saba na kupoteza tisa wakifanikiwa kufunga goli 31 huku wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 19.

Amesema, katika mechi zao zilizosalia, wana uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi na kupanda katika nafasi za juu zaidi kwani bado vijana wao wana hari ya kupambana.

“Kutolewa katika michuano hii hakutufanyi tukate tamaa bali kunatupa hasira zaidi ya kupambana ili kuweza kufanya vizuri katika mechi zetu zilizosalia za Ligi Ku una kuweza kupanda zaidi kutoka katika nafasi ya tano tuliyopo sasa,”.