Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Dodoma
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kuhakikisha wanayatoa magari yote yaliyotelekezwa na wamiliki wake katika karakana zote nchini na kusababisha mrundikano ndani ya karakana hizo.
Akizungumza na Menejimenti ya Wakala huo jijini Dodoma, Waitara amesema hatua hiyo itafanya kupunguza msongamano katika karakana hizo na hivyo kupatikana kwa nafasi, ili kuruhusu magari mengine kupata huduma kiurahisi.
“Magari hapa ni mengi na mrundikano ni mkubwa, mengine yanaonekana ni ya muda mrefu, hakikisheni mnayatoa na kuyapeleka kwa wenyewe ili kupunguza msongamano hapa na hata katika karakana zenu nyingine nchi nzima”, amesema Waitara.
Waitara ameutaka Wakala huo, kuboresha huduma zao nchi nzima ikiwemo kutatua mianya yote inayosababisha uhujumu na kufanya utendaji wa kusuasua kwa watumishi wa Wakala huo.
“Hakikisheni kuwa mnapunguza gharama, mnatumia muda mfupi na vipuri sahihi katika utengenezaji wenu wa magari, mkifanya hivi mtapunguza malalamiko kutoka kwa washitiri wenu,” amesisitiza Waitara.
Pia ameagiza Wakala huo, kuhakikisha wanatafuta njia sahihi ya kuhifadhi mafuta machafu yanayomwagika wakati wa utengenezaji wa magari, ili kuhifadhi mazingira katika maeneo yao ya kazi.
Kuhusu suala la vivuko, Waitara ameutaka Wakala huo kuhakikisha kila kivuko kinajisimamia na kujiendesha kwa faida na kutaka Wakala huo, kupitia upya tozo za nauli za vivuko nchini katika baadhi ya maeneo bila kuumiza wananchi.
“Huduma za serikali hazitakiwi kufanywa kwa kubahatisha kwa mfano katika Kivuko cha Nyamisati utaratibu wa safari na nauli haueleweki, wananchi wa huko wanalalamika sana, kaeni mlirekebishe hili, serikali haitaki watu wababaishaji,” amefafanua.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Heriel Mteri amesema Wakala unakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikwemo wakala kuendesha baadhi ya vivuko vyenye mapato madogo na hivyo kushindwa kujiendesha vyenyewe na kusababisha Wakala kutoa ruzuku ya kuviendesha.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni uchakavu wa miundombinu na vifaa vya karakana ambapo amesema, karakana hizo zimejengwa miaka mingi iliyopita hivyo kuhitaji ukarabati mkubwa.
Ameongeza kuwa kwa sasa, Wakala unatumia mfumo wa kisasa wa kubaini vipuri ambavyo si halisi katika karakana zake zote, ili kudhibiti udanganyifu ambao unafanywa na baadhi ya wafanyabiashara.
Naibu Waziri huyo, amefanya ziara TEMESA jijini Dodoma ili kujionea utendaji wa wakala na kuzungumza na Menejimenti kuhusu namna ya kuboresha huduma katika wakala huo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa