Na Daud Magesa,Timesmajira Online. Arusha
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amewapongeza watumishi wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Arusha kwa kukamilisha miradi ya kitaifa ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 82.5 kwa kiwango cha lami ambazo zimegharimu sh. bilioni 189.141.
Miradi hiyo ya barabara imejengwa na serikali kupitia wakala huo mkoani Arusha kwa gharama ya sh. bilioni 189.141 na kwamba, imekamilika kulingana na thamani ya fedha kwa kuzingatia mikataba ya ujenzi wake.
Akizungumza na watumishi wa TANROADS mkoani Arusha jana baada ya kukagua barabara hizo Naibu Waziri huyo amewapongeza kwa kusimamia vyema miradi hiyo ya ujenzi wa barabara na kuhakikisha, inakamilika kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mikataba ya ujenzi, pia kuhakikisha barabara zote wanazozisimamia mkoani hapa zinapitika majira yote ya mwaka.
“Niwahakikishie kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu, Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara iliyopo, pia miradi mipya itakayotengewa fedha kwenye bajeti ya serikali katika mwaka wa fedha wa 2021/22, nayo itatekelezwa,” amesema.
Miradi hiyo ya barabara ya Sakina-Tengeru (njia nne) kilomita 14.1, barabara ya mchepuko wa Kusini (Arusha Bypass) kilomita 42.4 na ujenzi wa barabara ya Kia hadi Mererani na zote zimekamilika kwa asilimia 100.
Akitoa taarifa ya miradi hiyo kwa Naibu Waziri huyo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Johnny Kalupale amesema barabara ya Sakina hadi Tengeru imegharimu sh. bilioni 70.365.
Amesema barabara ya mchepuko wa Kusini imejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 86.778 huku barabara ya Kia hadi Mererani, ikigharimu sh. bilioni 32 na kufanya jumla ya fedha zilizotumika kujenga barabara hizo kufikia sh. bilioni 189.141.
Mhandisi Kalupale amesema wakala huo, unaendelea na usimamizi wa miradi ya ujenzi wa barabara za Mto wa Mbu-Loliondo yenye urefu w kilomita 49, Kijenge-Usariver kilomita 20 na ujenzi wa mzani wa kisasa wa kupima uzito wa magari katika eneo la Kimokouwa katika barabara ya Namanga pamoja na kuendeleza ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Sakina hadi Tengeru, urefu wa kilomita 9.3.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti