Na Irene Clemence, TimesMajira Online, DSM
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulenya (DCEA), inawashikiria watu watatu akiwemo Balozi wa nyumba 10 katika mtaa wa Juwaje kunduchi Pwani, Kulwa Shamas(49) kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za Kulenya .
Watahumiwa wengine waliotajwa na (DCEA) ni Adadhati Mchongeza(20), Emmanuel Msakuzi (23) ambao kwa pamoja wamekamatwa na maofisa wa Mamlaka hiyo, wakiwa wameifadhi dawa aina ya heroin zenye ujazo wa gramu 400 pamoja na majani ya bangi puli moja katika mfuko wa nailoni.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam mapema Leo, kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, James Kaji amesema, watuhumiwa hao walikamatwa Januari 22 mwaka huu katika eneo la kunduchi Pwani Kauzeni Jijini Dar es salaam wakiwa na unga unaodhaniwa kuwa dawa za kulevya aina ya heroin sambamba na majani makavu ya bangi puli moja sawa na kete 30 za bangi.
“Maofisa wa DCEA walifanikiwa kufanya upekuzi na kisha kukamata dawa hizo zikiwa zimeifadhiwa ndani ya mfuko wa nailoni”amesema Kamishna Jenerali Kaji.
Amesema kuwa, Mamlaka hiyo inaendelea kuwashikiria watuhumiwa hao na kufikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Kamishna Jenerali Kaji amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Mamlaka hiyo ili DCEA iendelee kufanya kazi ya kukomesha vitendo hivyo.
Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali Kaji amesema katika kipindi mwezi Novemba mpaka Disemba mwaka jana DCEA imefanikiwa kushinda kesi tatu mahakamani zinazohusisha mapapa wa dawa za kulevya nchini ambao wamefungwa jela kwa miaka tofauti tofauti.
Akitaja majina ya mapapa hao ni pamoja na mfanyabiashara maarufu Jijini Tanga Yanga Omary Yanga maarufu Rais wa Tanga na kuhukumiwa miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin uzito wa gramu 1052.63
Mwingine ni Ayubu Mfaume maarufu kiboko ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa kosa la kusafirisha heroin uzito gramu 251.25.
Ameongeza kuwa, watuhumiwa wengine ni Raia wa Iran ambao walitiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye ujazo wa gramu 111.02 katika bandari ya Hindi ambapo mpaka sasa wanatumikia kifungo cha miaka 30.
Vilevile amesema, DCEA imefanikiwa kufungua vituo vitatu vya kutolea tiba ya methadone katika mkoa wa Tanga , Bagamoyo, pamoja na hospital ya Tumbi Pwani.
“Mamlaka imeogeza wigo wa upatikanaji wa tiba ya uraibu wa dawa za kulevya kwa kuongeza vituo vingine vitatu vya kutolea tiba ya methadone,” amesema Kamishna Jenerali Kaji.
Na kuongeza kuwa vipo katika maeneo ya segerea, Mbagala rangi tatu na Tegeta kuanza kutoa huduma Februari mwaka huu .
Pia amesema, mpaka sasa DCEA inaendelea Kudhibiti vitendo vinavyojiusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kiasi kikubwa.
“Sisi hatuna mchezo katika suala la kukamata watu wanaojiusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya tukikukamata unakwenda jela”amesisitiza Kamishna Jenerali Kaji.
Aidha amebainisha kuwa, DCEA inaendelea kutoa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa njia mbalimbali ikiwemo matukio makubwa ya kitaifa pamoja na vyombo vya habari.
“Mamlaka imeandaa mwongozo wa uelimishaji kwa wadau wanaofanya uelimishaji kwa makundi mbalimbali ya kijamii unaotarajia kukamilika mwishoni mwa mwaka huu wa fedha,”amesema Kamshina Jenerali Kaji.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato