November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Secretary-General Ant—nio Guterres swears in Mr. David Beasley (Executive Director, World Food Programme).

Ripoti yabainisha hofu ya Dunia kukumbwa na njaa

Na Mwandishi Wetu, NEW YORK

Mataifa mbalimbali duniani yametakiwa kuchukua tahadhari kubwa kutokana na hofu ya baa la njaa inayotarajiwa kuikumba Dunia.

Hayo yalibainishwa katika ripoti mpya iliyotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, Muungano wa Ulaya na Shirika la Marekani la Msaada wa Kimataifa (USAID). Ripoti inaonyesha kwamba, janga la mlipuko wa virusi vya corona (COVID-19) linaweka njia panda mustakabali wa chakula na lishe.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya pamoja ya kila mwaka kuhusu mgogoro wa chakula na lishe iliyotolewa na muungano wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kushughulikia mzizi wa njaa na lishe, inaeleza kuwa, COVID-19 inatoa tishio jipya katika uhakika wa chakula na lishe.

Miongoni mwa mashirika hayo ni la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP),Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura (OCHA), Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Chakula na Kilimo (FAO),Umoja wa Ulaya (EU) na USAID.

Aidha, kupitia ripoti hiyo iliyopewa jina la muungano wa kimataifa dhidi ya mgogoro wa chakula inaonyesha kwamba, mwishoni mwa mwaka 2019 watu milioni 135 katika nchi 55 walikabiliwa na changamoto ya kutokuwa na uhakika wa chakula.

“Katika nchi 55 zenye mgogoro wa chakula zilizoangaziwa kwenye ripoti hii watoto milioni 75 walikuwa na matatizo ya kudumaa na milioni 17 waathirika wa tatizo la kupoteza uzito, kutokana na utapiamlo kwa mwaka 2019,”ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasema hiki ni kiwango cha juu sana cha kutokuwa na uhakika wa chakula na utapiamlo kilichoorodheshwa na mtandao huo tangu kutolewa kwa ripoti ya kwanza mwaka 2017.

Mwaka huo huo wa 2019 ripoti imewaweka watu milioni 183 katika daraja la pili la kutokuwa na uhakika wa chakula ambalo ni sawa na kukabiliwa na njaa kubwa na kuwa katika hatihati ya kutumbukia katika mgogoro wa chakula endapo watakabiliwa na zahama nyingine kubwa kama janga la COVID-19.

Zaidi ya nusu ya watu hao milioni 135 walioangaziwa katika ripoti hii wanaishi barani Afrika, milioni 43 Mashariki ya Kati na Asia na milioni 18.5 Amerika ya Kusini na Caribbea.

Nchi 10 zilizoathirika vibaya na kukosekana uhakika wa chakula mwaka 2019 ni pamoja na Yemen, Congo DRC, Afghanistan, Venezuela, Bolivia, Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan, Nigeria na Haiti.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kichocheo kikubwa cha hali hiyo ni pamoja na vita ambavyo vimewasukuma watu milioni 77 kwenye hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi yaliyowaathiri watu milioni 34 na kuyumba kwa uchumi ambayo kumewaacha watu milioni 24 bila uhakika wa chakula.

Ripoti imependekeza kuchukuliwa hatua madhubuti hivi sasa ili kuwaepusha watu milioni 265 kutoka katika nchi za kipato cha chini kutumbukia katika janga kubwa zaidi la kutokuwa na uhakika wa chakula na baa la njaa.

Aidha, katika kikao maalum cha baraza la Usalama kilichofanyika juzi kwa njia ya mtandao ili kutathimini migogoro na uhakika wa chakula mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), David Beasely alisema,Dunia sio tu kwamba inakabiliwa na janga la kimataifa la afya, lakini pia janga la kimataifa la kibinadamu.

“Ukweli ni kwamba muda unatutupa mkono, hivyo hebu na tuchukue hatua kwa busara na kwa haraka. Ni muhimu sana kuja pamoja kama jumuiya ya kimataifa kupambana na janga hili la COVID-19,Ă®alisema Beasely.

Alisema, janga hilo limesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu tangu vita vya pili vya Dunia hasa ukizingatia kwamba dunia tayari inakabiliwa na dhoruba kubwa kuanzia mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili, vita, njaa na mengineyo.

Wakati huo huo, WFP imeliomba Baraza la Usalama kuongoza njia katika juhudi za kimataifa za kupambana na COVID-19.

Beasley alisema, jambo la kwanza wanahitaji amani, amewataka wote wanaohusika katika mapigano kuruhusu na kutoa fursa kwa wahudumu wa misaada ya kibinadamu kuzifikia jamii zisizojiweza na kuratibu msaada wa kuokoa maisha.

Sambamba na dola milioni 350 za ufadhili mpya ili kuweka mtandao wa kiufundi kuhakikisha mnyororo wa kimataifa wa usambazaji msaada unaendelea.

ìEndapo hatutajiandaa na kuchukua hatua sasa kupata fursa ili kuepuka pengo la ufadhili na usumbufu katika biashara huenda tukakabiliwa na baa la njaa kama lililoelezwa kwenye Biblia katika miezi michache ijayo,”alisema Beasley.

Naye Mkurugenzzi Mkuu wa Shirika la FAO, Qu Dongyu alizungumzia jinsi gani ripoti ya kimataifa ya mgogoro wa chakula ya 2020 ina uhusiano na migogoro na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula.

“Hatua za pamoja zinahitajika miongoni mwa wadau wa masuala ya kibinadamu, maendeleo na amani kushughulikia mizizi ya tatizo sugu la kutokuwepo kwa uhakika wa chakula,”alisema.

Pia alisema,utabiri wa uhakika wa chakula 2020 si mzuri na hivyo ni muhimu kuwa na tahadhari ya mapema na kuchukua hatua haraka kuzuia kutokuwa na uhakika wa chakula kunakosababishwa na migogoro katika maeneo mbalimbali.