November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri zatakiwa kuwa na miundombinu bora ya taka

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu amezielekeza halmashauri zote nchini kuwa na miundombinu bora ya kukusanya, kuhifadhi na kusafirisha taka ili kulinda afya za wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu akisikiliza maoni ya wafanyabiashara aliowakuta katika soko la Majengo jijini Dodoma wakati alipofanya ziara ya kushtukiza ya kukagua mfumo na miundombinu ya kushughulikia takangumu katika soko la majengo jijini Dodoma

Ummy ametoa maelekezo hayo jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika soko la Majengo jijini Dodoma kwa lengo la kuangalia mfumo mzima wa kushughulikia taka ngumu.

Katika ziara hiyo akiwa ameambatana na watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya Mazingira,Waziri Ummy ameonesha kuridhishwa na hali ya mazingira sokoni hapo na kuipongeza halmashauri ya jiji hilo.

Akizungumza mara baada ya kukagua soko hilo amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatoa kandarasi kwa watu wa kukusanya na kusafirisha taka wenye vifaa bora kwa ajili ya kazi hiyo.

Waziri huyo amesisitiza kuwa kutafanyika ukaguzi wa kuona kama wakandarasi hao wana vigezo na sifa zikiwemo kuwa na vifaa vya kuwakingia watumishi wanaokusanya taka.

“Tumeona gari za kukusanya na kusafrisha taka zenyewe zikiwa ni takataka kwa hiyo tutakagua kila halmashauri wajitathmini je, kandarasi hii waliyompa mtu wa kukusanya, kuhifadhi na kusafirisha taka ana vifaa bora. Hizi ni salamu tu tunataka masoko yawe safi na salama kwa wanaouza na wateja, kikubwa tunasema mazingira safi na salama kwa ajili ya maendelevu,” amesisitiza Ummy.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Ummy Mwalimu akisikiliza maoni ya wafanyabiashara aliowakuta katika soko la Majengo jijini Dodoma wakati alipofanya ziara ya kushtukiza ya kukagua mfumo na miundombinu ya kushughulikia taka ngumu katika soko la majengo jijini Dodoma jana. (Mpiga Picha Wetu).

Aidha,amesisitiza pawepo na utaratibu wa kuondoa taka zinazokusanywa na kuhifadhiwa kwenye masoko kwa wakati na kuwa hatavumilia kuona halmashauri yoyote ambayo takataka zinakaa kwa zaidi ya siku moja hatua itakasaidia kulinda afya za watumiaji wa masoko.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake inazitaka halmashauri zote za majiji, manispaa, miji na wilaya kuweka mifumo bora ya kukusanya, kuhifadhi na kusafirisha taka.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa taka ngumu Jijini la Dodoma, Dickson Kimaro alisema wana changamoto ya kypotea kwa vifaa wanavyopewa vibarua na kuahidi kuendelea kutoa vifaa vifaa hivyo.

Afisa Afya wa Kata ya Majengo,Yusta Maguzu amempongeza Waziri Ummy kwa ziara hiyo na kuahidi kuendelea kusimamia vyema mazingira katika kata yake ili kusaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko.