November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto wanaojihusisha na ugaidi hatarini

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao hawajiingizi kwenye makundi ya kigaidi, vinginevyo yatakayowakuta wasije wakailaumu Serikali.

IGP Sirro ametoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na utendaji kazi wa Polisi kwa mwaka 2020 na malengo waliyojiwekea kwa mwaka huu.

Onyo hilo la IGP Sirro kwa wazazi na walezi limekuja kufuatia swali aliloulizwa kuhusiana na hali ya usalama ilivyo mkoani Mtwara, ambako hivi karibuni kumetokea matukio yenye sura ya kigaidi.

“Kule Mtwara tunaenda vizuri, timu zetu zipo na ninawashukuru sana wananchi kule mpakani wanatupa taarifa vizuri, na huku ndani wanaofanya chokochoko wananchi wanatupa taarifa na tunawashughulikia vizuri,” amesema Sirro na kuongeza;

“Nitoe wito kwa wazazi na walezi kujitahidi sana watoto wao wasijiingize kwenye hayo makundi (kigaidi) kwa maana wakiishajiingiza kwenye makundi hayo hawatailaumu Serikali” amesema.

Amesisitiza kwamba hawana mchezo na watu wanaojiingiza kwenye ugaidi. “Ukishajiingiza kwenye ugaidi maana yake hiyo ni vita na ukiishajiingiza kwenye vita pia matokeo yake yanakuwa mabaya,” alisema Sirro na kuongeza;

“Ukiishaingia huko tukipambana utakayoyapata usilaumu, umetaka mwenyewe, ndiyo maana niliwaambia siku moja mama mtunze mwanao, maana akina mama ndiyo wana uchungu na watoto.

Kwa hiyo mama mtunze mwanao, kumtunza sio kumpa chakula tu, ni pamoja na kuhakikisha haiingii kwenye hayo makundi ambayo mwisho wa siku atapata tabu” amesema.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za mmoja wa wanaharakati kukamatwa, IGP Sirro alisema hata mwanaharakati anaweza kuwa gaidi, lakini huyo anayeitwa mwanaharakati watu wa Uhamiaji ndiyo wanashughulika naye, maana suala lake linahusu watu hao, lakini wao (Polisi) sio la kwao sana.

IGP Sirro, alionesha msisitizo wa ubaya wa vitendo vya kigaidi, alisema; “Hata ukiwa ni Sheikh au Padre hata kama ulikuwa ni Katekista gani ukiingia kwenye ugaidi, wewe ni gaidi utashughulikiwa kama gaidi mwingine. “Habari ya kuniambia wewe ni padre hizo hakuna.”