Na Rose Itono,TimesMajira Online,Mkuranga
WAATHIRIKA zaidi ya 1,000 wa mgogoro wa ardhi kwenye shamba namba 271 lililopo kati ya kijiji cha Lugwadu na Magodani wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani wamemuomba Rais Dkt.John Magufuli kuangalia upya mgogoro huo kwa kuwa maagizo aliyowaagiza wasaidizi wake yanakwenda tofauti.
Akizungumza na Majira jana wilayani Mkuranga Mwenyekiti wa Kamati ya Mgogoro wa shamba hilo Abdala Ndogondogo amesema hakuna muathirika hata mmoja aliyeshirikishwa kwenye mgao unaoendelea kufanywa na ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri pamoja na kuwepo na uasili wa kuishi katika eneo hilo na huku nyumba zao zikiwa zimebomolewa pasipo fidia yeyote.
Hivi karibuni rais akitokea Lupaso alimuagiza aliyekuwa Waziri wa Ardhi katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano William Lukuvi kurejesha ardhi hiyo kwa wananchi ili waendelee na shughuli zao jambo ambalo lilifanyika huku waathirika wakiwa njia panda kwa kutoshirikishwa kwa lolote.
Ameongeza kuwa maagizo aliyoyatoa rais Magufuli akitokea kijijini Lupaso kumzika marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu,Benjamin Mkapa la kumtaka Lukuvi kushughulikia mgogoro huo linakwenda tofauti kwa Halmashauri ya Mkuranga kutoishirikisha kamati ya waathirika wa mgogoro kwenye zoezi la ugawaji.
“Pamoja na ekari 750 kati ya 1,750 kurudishwa kwa wananchi bado kuna sintofahamu kwa sisi waathirika kwenye mgogoro huo kupata haki zetu kwani hakuna kiongozi yeyote wa halmashauri aliyetuita na kujua namna gani tutapata haki zetu,”alisema Ndogondogo na kuongeza kuwa katika kipindi cha mgogoro kuna nyumba za waathirika zilibomolewa.
Aidha ameongeza kumuomba rais kuuangalia upya mgogoro huu kwa kuwa umelenga kuwaacha wahusika njia panda na kuwaneemesha watu wengine kwenye ugawaji wa viwanja kijijini Lugwadu.
Awali mgogoro huu baina ya wananchi wa kijiji cha Lupasu na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Soap and Allied Industries ulidumu kwa zaidi ya miaka mitano ambapo ekari 750 zilirudishwa kwa wananchi na Serikali iliagiza zigawiwe kwa wahusika ambao ni wazawa kwa ushirikiano wa uongozi wa Halmashauri ya Mkuranga,Serikali ya kijiji na wazee wazawa jambo ambalo Kamati ya wahanga inalilalamikia kwa kutoshirikishwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mhandisi Mshamu Munde amesema ugawaji wa shamba hilo unazingatia maelekezo ya barua kutoka kwa aliyekuwa Waziri mwenye dhamana ya ardhi na kwamba haitokwenda kinyume.
Mhandishi Munde amesema barua hiyo haikuwaonesha wala kuelekeza kushirikisha kikundi chochote kwenye zoezi la ugawaji na kwamba endapo kuna malalamiko yeyote kwenye zoezi hilo ni vema wahusika wakafuata taratibu kwa kuzifuata mamlaka husika kutoa malalamiko yao.
“Mgogoro huu ni mrefu sana na kwa asiyeufahamu ataona kuna hujuma lakini ukweli uliopo kuna taratibu za uuzaji wa eneo kwa mwekezaji katika ngazi ya kijiji hazikufuatwa,”alisema Mhandisi Munde na kuongeza kuwa,viongozi wa kijiji wakati wakiuza eneo hilo hawakuwashirikisha wananchi kupitia mkutano wa kijiji.
Amesema Serikali kupitria halmashauri itagawa eneo hilo kwa mujibu wa taratibu na maelekezo yaliyotolewa na yeyote mwenye malalamiko anashauriwa kwenda kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kutoa malalamiko kwani serikali ya sasa ni sikivu.
Awali Rais Magufuli wakati akitokea kijiji cha Lupaso kumzika marehemu Rais wa Awamu ya Tatu alisimama Mkuranga kuzungumza na wananchi ambapo walimweleza kuhusiana na mgogoro huo uliodumu miaka mitano na kumtaka aliyekuwa Waziri wa Ardhi kuirudisha ardhi kuirudisha kwa wananchi hekari 750 kwa wananchi ambao walikuwa tayari wanaishi eneo hilo na mwekezaji kuhaki na hekari 1000 badala ya kuwaondoa.
More Stories
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi