November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kituo cha Ufaransa Alliance chaandaa Maonesho

Na David John, TimesMajira Online

KATIKA kuelekea kwenye sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya, Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa Alliance kimeandaa maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiriamali ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wajasiriamali hao kukutana na wateja wapya.

Kituo hicho ambacho kipo chini ya Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania kimeweka wazi kuwa kinaamini kupitia maonesho hayo wajasiriamali wakiwemo wale wanaouza bidhaa za mkono ambazo zimetokana na ubunifu wa kitanzania utakwenda kukuza soko la bidhaa hizo kutokana na kukutanishwa na watu kutoka sehemu mbalimbali waliofika kwenye maonesho hayo.

Wakizungumza na Mtandao wa TimesMajira na TimesMajira TV, wakati wa maonesho hayo ya siku moja, baadhi ya wajasiriamali wametoa pongezi kwa Kituo cha Utamaduni cha francies Alliance kwa kuandaa maonesho hayo kwani pamoja na mambo mengine imekuwa fursa kwao kutanua wigo wa kibiashara.

Akizungumzia maonyesho hayo mjasiliamali Getrude Mtallo kutoka Duka la Chema Design linalojihusisha na uuzaji wa bidhaa za nguo amesema, maonyesho hayo yamewasaidia kuwakutanisha na wateja wapya hasa kipindi hiki cha kuelekea msimu wa sikukuu.

Amesema, katika naonyesho hayo walikuja na bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo mapanzia pamoja na bidhaa zingine za mapambo ya ndani, hivyo ametoa shukrani kwa waandaaji wa maonesho.

“Sis tupo hapa hapa jijini Dar es Slaam katika maeneo ya Oyesterbay na kimsingi kwenye maonesha haya tumefanya biashara kidogo, lakini chakufurahisha tumebadilisha mawasiliano na wateja.Ushauri wangu maonesho haya yawe yanafanyika mara kwa mara na yawe yanatangazwa ili kutoa fursa ya watu wengi kushiriki,”amesema Getrude.

Kwa upande wake mjasiliamali Pili Mohamed amesema, maonesho hayo yaliyofanyika kwenye kituo cha Utamaduni cha Ufaransa Alliace wanashukuru wamefanya biashara kidogo tofauti na wasingefika kabisa.

Pili ambaye anafanya shughuli zake za ujasiriamali maeneo ya Sleep Way jijini Dar es Salaam ameweka wazi amefurahi kupata fursa ya kushiriki kwenye maonesho hayo.

Naye mfanyabiashara Salvina Richard amesema, baada ya kumalizika kwa maonyesho hayo, sasa anarudi kwenye maeneo yake ya biashara ya kila siku yaliyopo Coast Furniture and Hand Craft Masaki huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kutembelea katika biashara zake kuona bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.

Awali mwanamziki na mmiliki wa bendi ya bendi ya Seghito Afro Jazz, Aneth Ngongi aliyekuwa akitoa burudani wakati wa maonesho hayo, amesema Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania kupitia kituo hicho cha utamaduni wamekuwa na moyo mkubwa wa kuwasaidia wasanii na wanamuziki wa Tanzania, hivyo nao wanalojukumu la kuendelea kushirikiana nao.

“Pamoja na kuwepo kwa maonesho ya bidhaa mbalimbali, kwetu sisi tumepata fursa ya kutumbuiza watu waliokuwa wanakuja hapa kununua na kuangalia bidhaa zenye ubora.Naamini burudani ambayo tumeitoa itakuwa imewakuna wengi kwani hata sisi tumefurahi kuwepo hapa siku ya leo.Tunafahamu katika kuelekea msimu wa sikukuu kituo kimeona umuhimu wa kuwakutanisha wajasiriamali na wateja wao,”amesema.

Kuhusu bendi yake, amesema tangu imeanzishwa imefikisha miaka nane, na amekuwa akishirikiana a Kituo cha Utamaduni ya Ufaransa Alliance kwa miaka saba sasa, na hasa kila wanapopata mualiko huku akitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kujenga utamaduni wa kutembelea kituo hicho kwani hakuna kiingilio chochote kwa wanaotaka kwenda kushuhudia burudani.