November 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Chande azindua bweni la Wasichana Chuo cha BTI

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande amezindua bweni la wasichana lililopo katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora (BTI) lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 150 kwa wakati mmoja lililojengwa kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).

Akizindua bweni hilo lililopewa jina la Dkt. Ashatu Kijaji ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii,Chande amewataka wanafunzi wa chuo hicho kutumia vyema miundombinu iliyopo kwenye bweni hilo ili liendelee kuwa na mvuto kwa wengine na kuonesha thamani ya fedha zilizotumika katika ujenzi wake huku akielekeza chuo hicho kujenga bweni la wanaume.

Aidha,Chande amepongeza na kushukuru Umoja wa Ulaya katika kusimamia ufadhili wa jengo hilo huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuthamini mchango unaotolewa na wadau wote wa maendeleo ikiwemo EU.

Awali Chande ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuendelea kuelekeza fedha kwa ajili ya shughuli za chuo na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia ikiwemo ujenzi wa jengo la mihadhara na maabara.

Chande amesema katika Mwaka wa Fedha 2026/2027 chuo kimeidhinishiwa bajeti ya Sh. bilioni 3.9 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo na shughuli nyingine huku akielekeza Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa samani na vitendea kazi kwa ajili ya jengo la mihadhara na maabara ya chuo hicho.