Na Mwandishi Wetu
KIUNGO wa klabu ya Yanga, Mukoko Tonombe, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba msimu wa 2020/21 huku kocha wake Cedric Kaze naye akichukua Tuzo ya Kocha Bora wa mwezi huo.
Mukoko na Kaze walitwaa tuzo hizo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa mwezi huo Oktoba, Yanga ilicheza mechi nne na kushinda zote jambo lililowawezesha kupanda hadi kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom inayoshirikisha timu 18 kwa kuifunga Coastal Union 3-0, Polisi Tanzania 1-0, KMC 1-2 na Biashara United 0-1 huku Mukoko alitoa mchango mkubwa katika ushindi huo ikiwa ni pamoja na kufunga bao moja dhidi ya Polisi Tanzania.
Katika kinyang’anyiro hicho, Mukoko aliwashinda mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube na mshambuliaji wa Gwambina FC, Meshack Abraham aliongia nao fainali, ambapo Dube aliiongoza Azam kubaki kileleni baada ya kuvuna pointi 10 katika mwezi huo, ikishinda tatu, sare moja na kupoteza moja, huku mshambuliaji huyo akifunga mabao matatu na kutoa pasi tatu za usaidizi wa mabao.
Meshack aliiongoza Gwambina kupata pointi nane ikishinda michezo miwili, sare miwili na kupoteza mmoja, ikipanda kutoka nafasi ya 17 hadi ya 14 akiifungia timu yake mabao manne.
Kwa upande wake Kaze aliwashinda Aristica Cioaba wa Azam na Francis Baraza wa Biashara United ambapo Kaze aliiongoza Yanga katika michezo mitatu na kushinda yote. Yanga chini ya Kaze ilizifunga Polisi Tanzania, KMC na Biashara United na kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili.
Cioaba aliiongoza Azam kushinda michezo mitatu, sare moja na kupoteza moja, huku Baraza akiiongoza Biashara kushinda michezo mitatu na kupoteza miwili ikipanda kutoka nafasi ya saba hadi ya nne.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025