Na Agnes Alcardo,Makambako
MKANDARASI anayetekeleza mradi wa maji katika Mji wa Makambako, mkoani Njombe, ametakiwa kuongeza kasi ya kazi ili kukamilisha ujenzi ifikapo Desemba 30, mwaka huu, baada ya mradi huo kufikia asilimia 85 ya utekelezaji wake.
Wito huo umetolewa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenan Kihongosi, aliyesisitiza kuwa wananchi wanahitaji kuona huduma ya maji ikiwafikia badala ya kuendelea kupewa maelezo kuhusu hatua za utekelezaji wa mradi.
Kihongosi amemtaka mkandarasi huyo kuongeza nguvu kazi, kuhakikisha vifaa vinapatikana kwa wakati na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha kazi. Amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo unapaswa kuendana na muda uliopangwa ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji huo.
Pia amesisitiza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika ujenzi huo, akieleza kuwa fedha zinazotumika ni za Serikali ya Tanzania hivyo ni muhimu matumizi yake yazingatie tija na thamani ya fedha.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Makambako, Yohana Mgaza, amesema mradi huo ukikamilika utaongeza upatikanaji wa maji katika mji huo kutoka asilimia 61.5 hadi asilimia 100, huku miundombinu yake ikitarajiwa kukidhi mahitaji ya wakazi kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.
Mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani Mil 8.8 unahusisha ujenzi wa miundombinu ya kuchukua na kusafirisha maji kutoka Mto Mbalali, mabomba ya usambazaji pamoja na matanki ya kuhifadhi maji, likiwemo tanki la lita milioni mbili katika eneo la Kiumba.
Aidha mradi huo ni sehemu ya mpango wa kuboresha huduma ya maji katika miji 28 nchini, unaohusisha pia Rujewa na Wanging’ombe. Kihongosi ameitaka Serikali ya wilaya kufuatilia kwa karibu kazi zinazoendelea ili kuhakikisha mkandarasi anakamilisha wajibu wake kwa muda uliopangwa.

More Stories
Jamii yatakiwa kuondoa dhana kukwamisha wanawake kushiriki michezo
Mwigulu kufunga maadhimisho ya wenye ulemavu Mwanza
Rais apongeza hatua makubaliano kupunguza vifo mama,mtoto