October 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCB, MAKAZI SOLUTIONS watanua fursa za umiliki wa viwanja

Na Mwandishi wetu,TimesMajira

KAMPUNI ya Makazi Solutions Limited imeingia makubaliano ya ushirikiano na Benki ya TCB kwa lengo la kuwawezesha wananchi kumiliki viwanja vilivyopimwa kwa kulipa kidogo kidogo, hatua inayolenga kupunguza changamoto za upatikanaji wa ardhi na kuimarisha makazi bora nchini.

Makubaliano hayo yanalenga kuwawezesha wananchi kupata mikopo ya kununua viwanja bila kulazimika kulipa gharama zote kwa wakati mmoja, huku wakipata fursa ya kutumia huduma za kifedha za TCB kulingana na masharti ya mikopo husika.

Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo, Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Msham Munde, amempongeza Makazi Solutions Limited kwa kuanzisha mpango huo, akisema unadhihirisha mchango wa sekta binafsi katika kutatua changamoto za makazi na kusaidia wananchi kumiliki ardhi iliyopangwa na kupimwa.

“Niwapongeze sana Makazi Solutions Limited kwa miradi mnayoifanya. Nimefahamishwa kuhusu shughuli zenu, na ninafurahi kuona kampuni hii ya wazawa, inayoendeshwa na vijana, ikichangia katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi,” amesema Munde.

Amesema Serikali inaendelea kuhimiza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kutekeleza miradi ya maendeleo, hususan katika kuboresha makazi na kupunguza ujenzi holela.

“Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni zinazotekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi. Mipango kama hii inaendana na jitihada za maendeleo ya taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Makazi Solutions Limited, Suleiman, amesema kampuni hiyo yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15 imeingia makubaliano hayo ili kurahisisha upatikanaji wa viwanja na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi katika kumiliki ardhi.

“Tumelenga kurahisisha upatikanaji wa viwanja kwa wananchi kwa kuwawezesha kulipa kwa awamu. Tunatambua kuwa wananchi wana mahitaji mengi ya kifamilia, hivyo utaratibu huu utawasaidia kupanga matumizi yao ya fedha huku wakitimiza ndoto ya kumiliki ardhi,” amesema Suleiman.

Amesema changamoto ya makazi nchini inahitaji mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi, akieleza kuwa ujenzi holela unaweza kusababisha matatizo ya miundombinu, migogoro ya ardhi na ugumu wa kupata huduma za kifedha.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo unalenga kuwapa wananchi fursa ya kulipia viwanja kwa awamu ili waweze kutimiza mahitaji mengine muhimu ya familia zao huku wakielekea kumiliki ardhi.

Aidha, ameomba TCB kupanua ushirikiano huo kwa kuangalia uwezekano wa kufadhili ununuzi wa maeneo makubwa ya ardhi, ambayo yanaweza kupangwa na kuendelezwa kuwa makazi bora badala ya kutoa mikopo kwa wanunuzi wa viwanja pekee.

“Tunaomba ushirikiano huu uende hatua nyingine kwa kuangalia uwezekano wa kufadhili ununuzi wa maeneo makubwa ya ardhi, ambayo yatapangwa na kuendelezwa kuwa makazi bora. Hatua hiyo inaweza kuongeza upatikanaji wa viwanja vilivyopimwa na kupunguza ujenzi holela,” amesema.

Amesema utaratibu huo unaweza kusaidia kuongeza upatikanaji wa ardhi iliyopimwa, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na halmashauri kupitia kodi na ada mbalimbali, pamoja na kupunguza migogoro inayotokana na umiliki usio rasmi wa ardhi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa Wateja Wadogo na wa Kati wa TCB, Francis Kaaya, amesema benki hiyo iko tayari kushirikiana na Makazi Solutions Limited katika kuwawezesha Watanzania kupata ardhi na kutimiza ndoto ya kumiliki makazi bora.

“TCB iko tayari kushirikiana na Makazi Solutions Limited katika kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi na kufikia malengo yao ya kuwa na makazi bora,” amesema Kaaya.

Amewahimiza wananchi na wafanyabiashara wenye nia ya kununua viwanja kuwasiliana na benki hiyo kupitia matawi yake yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini ili kupata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa.

Amesema TCB inaendelea kutumia mtandao wake wa matawi kuwafikia wananchi wanaohitaji huduma za kifedha, wakiwemo wafanyakazi na wafanyabiashara wanaotaka kununua viwanja au kurasimisha umiliki wa ardhi.