Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka nchi za Afrika kuimarisha usimamizi wa Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) ili kulinda fedha za wanachama, kuongeza imani ya wananchi na kuvifanya vyama hivyo kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii
Akizungumza katika Kongamano la Kimataifa la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Barani Afrika (SACCA Congress 2026), lililofanyika leo jijini Dar es Salaam, Dkt.Mwigulu amesema usimamizi madhubuti ni muhimu katika kujenga uaminifu na kuhakikisha taasisi hizo zinaendelea kutoa huduma bora kwa wanachama.
Amesema SACCOS zinapaswa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa fedha, usimamizi wa mtaji na ubora wa mali, huku serikali, wasimamizi wa sekta ya fedha na wadau wa ushirika wakishirikiana kuimarisha utawala bora na usalama wa mifumo ya kidijitali.

Dkt. Nchemba amesema SACCOS ni nyenzo muhimu za maendeleo kwa kuwa zinawezesha wakulima kugharamia uzalishaji, familia kusomesha watoto, wanawake kuanzisha biashara na vijana kubadilisha mawazo ya kibiashara kuwa miradi inayozalisha kipato na ajira.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amezitaka SACCOS kubuni huduma za kifedha zenye gharama nafuu zinazokidhi mahitaji ya kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na biashara. Amesema huduma hizo zinapaswa kuwawezesha wakulima kupata pembejeo, teknolojia za kisasa, mitambo ya kilimo na masoko ya mazao.

Chongolo amesema hadi mwisho wa mwaka 2025, Tanzania ilikuwa na SACCOS 981 zilizohudumia takribani wanachama milioni 1.9, huku mali za vyama hivyo zikifikia Sh trilioni 1.669, ikiwa ni ongezeko la karibu asilimia 60 ndani ya mwaka mmoja.
Naye Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Shirikisho la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Afrika (ACOSCA), Dkt. Samuel Nyarko,amesema atajikita katika kuimarisha utawala wa taasisi, kupanua ushirikiano wa kimkakati na kuongeza ushawishi wa Afrika katika majukwaa ya kimataifa, huku akihimiza matumizi ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi.




More Stories
STAMICO yaimarika, yatekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R
Ndejembi aridhishwa na ujenzi wa Kituo cha Umeme Iganjo
Wizara ya Viwanda yabainisha utendaji wa taasisi zake