
Na Moses Ng’wat, Sumbawanga
MWENGE wa Uhuru mwaka 2026 umekamilisha ziara yake mkoani Songwe baada ya kukagua miradi 39 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 14, kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Rukwa.
Makabidhiano hayo yamefanyika, Oktoba 10, 2026, katika viwanja vya Kilyamatundu, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Abubakar Kunenge, amemkabidhi Mwenge huo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere.
Kwa siku sita tangu ulipopokelewa Mkoa wa Songwe Oktoba 5, 2026, Mwenge huo umekimbizwa umbali wa zaidi ya kilometa 600, huku miradi mbalimbali ikikaguliwa, mingine ikizinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amesema ameridhishwa na ubora wa miradi waliyotembelea, akiwapongeza viongozi na watendaji kwa usimamizi wake.
Amesema timu hiyo imejionea mwitikio mkubwa wa wananchi katika kupokea na kuukimbiza Mwenge, akieleza kuwa ushiriki huo unaimarisha umoja na kuwahamasisha kushiriki maendeleo.
Mwang’onda amesema Songwe imekuwa darasa kwao kutokana na mambo mazuri waliyojifunza, akiahidi kuyatumia kuboresha utekelezaji wa majukumu yao katika maeneo mengine.
Ametaja Daraja la Mto Isenga wilayani Ileje kuwa mfano wa utekelezaji wa maelekezo ya Mwenge, akisema baada ya kuagiza maboresho, wamebaini hatua kuchukuliwa haraka, ikiwamo uwekaji wa zege.
Kwa upande wake, Kunenge amewashukuru wananchi wa Songwe kwa kujitokeza kwa wingi katika mapokezi na mbio za Mwenge, akisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano katika kuharakisha maendeleo ya taifa.



More Stories
Kikwete atangaza Mkutano wa Rasilimaliwatu Afrika
AHF yatumia uwezeshaji kupunguza VVU
CRDB yavutiwa na ubunifu wa vijana VETA, yatoa zawadi