October 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabunge Afrika watakiwa kugeuza ahadi za Afya kuwa vitendo

Na Penina Malundo,TimesMajira

WABUNGE wa Afrika wametakiwa kutumia nafasi zao za kutunga sheria, kuidhinisha bajeti na kuisimamia Serikali kuhakikisha ahadi za kupunguza vifo vya kina mama na watoto zinageuzwa kuwa hatua halisi na matokeo yanayopimika katika jamii.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 8,2026 na Mwenyekiti wa Mtandao wa Kijiografia wa Afrika wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU Africa Geopolitical Group), ambaye pia ni Mbunge kutoka nchi ya Chad,Ali Tchaïmi wakati wa Mjadala wa Pamoja wa Kibunge kuhusu Afya ya Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto na Vijana, uliofanyika jijini Arusha.

Tchaïmi amesema Afrika tayari imeweka sera, mikakati na mpango wa pamoja wa kukabiliana na vifo vya mama na watoto, hivyo hatua inayofuata ni kuhakikisha ahadi hizo zinabadilika na kuwa huduma zinazowafikia wananchi, hususani walioko katika maeneo ya mbali na yaliyo hatarini.

Amesema mabunge yana jukumu kubwa katika kufanikisha ajenda hiyo kwa kuwa yana uwezo wa kutunga sheria, kuidhinisha bajeti na kusimamia utekelezaji wa sera za Serikali.

“Ni katika mabunge yetu ambako vita ya kufikia zile sifuri tatu inapaswa kushinda. Ni wajibu wetu kuhakikisha rasilimali zilizotangazwa kwa ajili ya afya zinapatikana na kutumika ipasavyo,” amesema.

Amezitaja sifuri tatu kuwa ni kuhakikisha hakuna kujifungua nyumbani bila msaada wa kitaalamu, hakuna kifo cha mama au mtoto mchanga kinachoweza kuzuilika na hakuna mtoto anayekosa chanjo.

Tchaïmi amesema pia ni muhimu kuhakikisha vituo vya afya vinakuwa na watumishi, dawa na vifaa vinavyohitajika, huku mapendekezo yanayotokana na uchunguzi wa vifo vya kina mama na watoto wachanga yakitumika kuchukua hatua za marekebisho.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma za chanjo zinamfikia kila mtoto bila kujali mahali anapoishi.

Katika hotuba yake, Tchaïmi ametoa mfano wa Chad, akisema Serikali ya nchi hiyo chini ya Rais Mahamat Idriss Déby Itno imeipa afya nafasi muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali, hususan afya ya mama na mtoto, chanjo na uimarishaji wa mfumo wa afya.

Amesema uongozi wa kisiasa wa ngazi ya juu ni muhimu katika kuhakikisha sera za afya zinatoa matokeo, akibainisha kuwa Rais wa Chad huongoza kikao cha kila mwezi cha kufuatilia sekta ya afya kinachowakutanisha Serikali na wadau mbalimbali.

Kwa mujibu wa Tchaïmi, uzoefu huo unaonyesha kuwa pale ambapo utashi wa kisiasa, rasilimali za umma na usimamizi wa mabunge vinaenda pamoja, nchi zinaweza kubadilisha mwelekeo wa viashiria vya afya.

Amesema Mtandao wa Kijiografia wa Afrika wa IPU unaweza kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na mbinu bora kati ya mabunge, pamoja na kuhakikisha sauti za jamii zilizo hatarini, hususan wanawake na watoto, zinakuwa sehemu ya maamuzi ya kisiasa.

Tchaïmi pia aliunga mkono Pendekezo la Hatua za Kibunge la Arusha, akisisitiza kuwa mkutano huo haupaswi kuishia katika kutoa tamko la kisiasa, bali uwe mwanzo wa hatua madhubuti katika mabunge ya Afrika.

“Arusha isiwe tamko la kanuni pekee. Arusha iwe alama ya kutoka katika maneno ya kibunge kwenda kwenye hatua za kibunge, ili kila Bunge lirudi nchini kwake na kuchukua angalau hatua moja ya konkrète, kisha turudi katika miezi ijayo kupima maendeleo yaliyofikiwa,” amesema.

Amesema Mtandao wa Kijiografia wa Afrika wa IPU uko tayari kushirikiana na Bingwa wa AU wa Afya ya Mama na Mtoto, Rais Samia Suluhu Hassan, Africa CDC, taasisi za kikanda na washirika wa maendeleo katika kuendeleza ajenda hiyo.

Tchaïmi amesema nyuma ya sifuri hizo tatu kuna ahadi tatu ambazo Afrika inapaswa kuzitimiza; kuhakikisha kila mama anajifungua kwa usalama, kila mtoto mchanga anapata nafasi ya kuishi na kila mtoto analindwa dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Afrika Kusini,Angela Didiza, amezitaka nchi za Afrika kuimarisha ufadhili wa ndani wa sekta ya afya na mabunge kuongeza usimamizi wa matumizi ya fedha ili huduma za afya ya mama, mtoto mchanga na chanjo ziwafikie wananchi, hasa familia zenye uhitaji mkubwa.

Amesema hali ya sasa ya ufadhili wa afya inahitaji hatua madhubuti za kisiasa kutokana na kupungua kwa nafasi ya kifedha katika nchi nyingi zinazoendelea.

“Ongezeko la majukumu ya kulipa madeni ya nchi limeendelea kubana uwezo wa Serikali kutenga fedha kwa huduma muhimu za kijamii, huku baadhi ya nchi zikikabiliwa na kupungua kwa misaada ya maendeleo kwa sekta ya afya.

“Bajeti za umma zinazidi kubanwa, na nchi nyingi zinazoendelea zinakabiliwa na majukumu makubwa ya kulipa madeni, hali inayopunguza nafasi ya kifedha kwa Serikali,” amesema.

Amesema katika mazingira hayo, wabunge wanapaswa kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa afya zinakuwa za uhakika na zinatumika kwa huduma muhimu, zikiwemo afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto pamoja na huduma za vijana.