October 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt Tulia: Mabunge yaweke nguvu kuboresha huduma za afya

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

RAIS wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, amezitaka nchi kupitia mabunge yao kuongeza nguvu katika kuboresha huduma za afya kwa wanawake, watoto na vijana ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

Amesema afya ya wanawake, watoto na vijana inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya mabunge, serikali na wadau mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuweka sera na sheria zinazolinda afya na ustawi wa makundi hayo.

Dkt.Tulia ameyasema hayo leo Oktoba 8,2026 wakati akizungumza katika Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaoendelea jijini Arusha, akihutubia mtandao wa wabunge unaohusika na masuala ya Afya ya Wanawake, Watoto Wachanga na Vijana.

Dkt.Tulia amesema changamoto zinazowakabili wanawake, watoto na vijana zinahitaji hatua za pamoja na endelevu, ikiwamo kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya, rasilimali za kutosha na uwajibikaji katika utekelezaji wa mipango ya afya.

Kwa mujibu wa Dkt. Tulia, amesema Mabunge yana nafasi kubwa ya kuhakikisha ahadi za kisiasa kuhusu afya zinageuzwa kuwa hatua na matokeo yanayoonekana katika jamii.

Amesema ushirikiano wa wabunge kutoka nchi mbalimbali kupitia IPU unaweza kusaidia kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora na kuimarisha usimamizi wa sera na mipango inayolenga kuboresha afya ya wananchi.

Dkt. Tulia amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya vijana katika huduma za afya, hasa afya ya uzazi na ustawi wao, akisema kundi hilo ni sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa.

Amesema mabunge yanapaswa kuendelea kutumia nafasi yao kutunga sheria, kutenga na kusimamia rasilimali pamoja na kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote kwa usawa.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, amesema mabunge yana nafasi kubwa katika kupunguza vifo vya akina mama, watoto na changamoto za afya kwa vijana kwa kuhakikisha kunakuwa na sheria zinazowezesha huduma bora za afya na rasilimali za kutosha.

Amesema afya na ustawi wa wanawake, watoto na vijana ni msingi muhimu wa maendeleo ya Tanzania, hivyo kila kifo kinachoweza kuzuilika na changamoto ya kutokuwepo kwa huduma muhimu za afya vinahitaji hatua za kisiasa na utekelezaji wa kudumu.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameweka msukumo wa kupunguza vifo vya akina mama na watoto hadi kufikia sifuri, si Tanzania pekee bali pia katika Bara la Afrika kupitia nafasi yake kama kinara wa Umoja wa Afrika (AU) katika masuala ya afya ya mama na mtoto.

“Bunge lina wajibu muhimu wa kusimamia sheria zinazosaidia, kuhakikisha kuna fedha za kutosha na zinazoeleweka, pamoja na kusimamia utekelezaji ili rasilimali ziwafikie watoa huduma na jamii zinazozihitaji zaidi,” amesema Zungu.

Aidha, amesema juhudi za nchi zinapaswa kulenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za afya kwa usawa, ikiwamo huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto mchanga, lishe pamoja na huduma za afya na ustawi wa vijana.

Zungu amesema kupitia mtandao huo, wabunge kutoka nchi mbalimbali wanaweza kubadilishana uzoefu, kuimarisha uwajibikaji wa mabunge na kuhamasisha hatua za vitendo katika nchi zao ili kuhakikisha ahadi za kisiasa zinabadilika kuwa matokeo ya kudumu kwa wananchi.