Na Penina Malundo,TimesMajira
MTAALAMU kutoka Kituo cha Kimataifa cha Utawala wa Akili Bandia (AI),Sekam Abdella ameiomba Serikali na mabunge kuhakikisha maendeleo na matumizi ya Akili Bandia (AI) yanaenda sambamba na ulinzi wa haki za wafanyakazi.
Amesema kuwa kuwaandaa watu kwa uchumi wa AI pekee bila kuweka mifumo ya ulinzi kunaweza kuongeza changamoto katika soko la ajira.
Sekam ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani IPU unaoendelea katika moja ya majadiliano ya Jopo kuhusu masuala ya AI.
Amesema ingawa AI inatarajiwa kuleta manufaa makubwa katika uchumi na kuongeza fursa za ajira, faida hizo zinaweza kutosambaa kwa usawa kutokana na tofauti katika miundombinu ya kidijitali, pengo la ujuzi na tofauti za kiuchumi zilizopo kati ya nchi.
Amesema serikali inapaswa kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali, elimu na kujenga uwezo wa wananchi ili kuwawezesha kunufaika na fursa zinazotokana na AI, huku zikichukua hatua za kuhakikisha teknolojia hiyo haiongezi pengo la kiuchumi duniani.
Akizungumzia matokeo ya Global Index on Responsible AI, Sekam amesema utafiti huo umeonyesha kuwa nchi nyingi zinafanya juhudi kubwa kuwajengea wafanyakazi ujuzi unaohitajika katika uchumi unaotumia AI, lakini bado kuna pengo katika sheria zinazolinda wafanyakazi dhidi ya hatari zinazoweza kutokana na matumizi ya teknolojia hiyo.

“Serikali inawafundisha wafanyakazi kwa ajili ya uchumi wa AI, lakini si lazima ziwe zinawalinda dhidi ya hatari na madhara yanayoweza kuambatana na AI,” amesema.
Amesema hali hiyo inaonekana zaidi katika nchi za Global South, ambapo asilimia 41 ya nchi zilizofanyiwa tathmini zina mipango ya kuwajengea wafanyakazi ujuzi mpya au kuongeza ujuzi, wakati ni asilimia 13 pekee zenye mifumo ya ulinzi wa wafanyakazi dhidi ya athari zinazohusiana na AI.
Kwa mujibu wa Sekam amesema baadhi ya wafanyakazi, hususan wanaofanya kazi za data kama uchambuzi na uwekaji wa taarifa, ukaguzi wa maudhui na uwekaji alama kwenye data, wanakabiliwa na mazingira ya kazi yasiyo na uhakika, malipo duni na changamoto za kiafya na kisaikolojia.
Amesema matumizi ya mifumo ya kiotomatiki katika kuajiri, kusimamia na kutathmini wafanyakazi nayo inapaswa kuwa wazi, ya haki na yenye nafasi ya mfanyakazi kupinga uamuzi unaofanywa na mfumo huo, huku maamuzi muhimu yakibaki chini ya usimamizi wa binadamu.
Amesisitiza kuwa mabunge yana nafasi muhimu ya kutunga sheria zinazotambua aina mpya za kazi zinazotokana na uchumi wa kidijitali, kuweka taasisi za usimamizi na kuhakikisha wafanyakazi wanapata fursa ya kujipanga na kudai haki zao kwa pamoja.
Kwa upande mwingine, amependekeza serikali iweke mkazo katika elimu na ujuzi wa AI kwa umma, sambamba na kuweka viwango vya kazi salama na zenye heshima ili ukuaji wa uchumi unaotokana na teknolojia hiyo uweze kuboresha maisha ya wafanyakazi.
Kwa upande wake, Mbunge na Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Majimbo la Afrika Kusini,Poobalan Govender amesema nchi nyingi zinazoendelea zinakabiliwa na ukosefu mkubwa wa ajira, ukosefu wa usawa na upatikanaji usio sawa wa elimu, miundombinu ya kidijitali na ujuzi wa teknolojia, hali inayoweza kufanya baadhi ya makundi kuathirika zaidi na AI.
Ametaja vijana wanaoingia katika soko la ajira, wanawake, wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi na wanaofanya kazi zinazojirudia kuwa miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kuathirika na mabadiliko ya kiteknolojia.
“Mustakabali wa ajira haupaswi kuachwa kwa nguvu za soko na wataalamu wa teknolojia pekee, bali mabunge yanapaswa kutumia mamlaka yao kupitia utungaji wa sheria, usimamizi na michakato ya bajeti kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanaendana na utu na haki za wafanyakazi,”amesema

More Stories
EWURA yawakumbusha wateja haki zao
Mwanga Hakika Benki yatoa upimaji macho bure
Mwenge waweka jiwe la msingi madarasa matatu Tunduma