October 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Louis-Olivier Favot Mkurugenzi Mtendaji Mpya wa Mixx

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online

MIXX Tanzania, imetangaza mabadiliko katika uongozi wake wa juu, huku Angelica Pesha akihitimisha safari yake ya zaidi ya miaka 15 katika kampuni hiyo huku Louis-Olivier Favot akiteuliwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya.

Mabadiliko hayo hayo yalifanyika juzi, ambayo yanaashiria mwisho wa safari ndefu ya Pesha katika kuijenga na kuiendeleza kampuni, tangu ilipoanza kama Tigo Pesa hadi kuwa kampuni kubwa ya teknolojia ya fedha (fintech) inayotoa huduma mbalimbali za kifedha kidijitali nchini Tanzania.

Louis-Olivier Favot, ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika huduma za benki, huduma ndogo za fedha, fedha kwa njia ya simu na huduma nyingine za kifedha za kidijitali.

Pesha aliteuliwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu mwaka 2020 na baadaye akaongoza kampuni katika kipindi muhimu cha mabadiliko kutoka Tigo Pesa hadi Mixx Tanzania.

Chini ya uongozi wa Pesha, Mixx iliendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza huduma za kifedha za kidijitali nchini, na kutambuliwa kwa mafanikio hayo kupitia tuzo mbalimbali za ubora na ubunifu.

Miongoni mwa tuzo hizo ni tuzo tatu ilizopokea katika Tuzo za TEHAMA mwezi Agosti 2026, zikiwemo Tuzo ya Ubunifu katika Huduma za Fedha kwa Njia ya Simu huku Pesha alitunukiwa Tuzo ya Uongozi wa Kike katika TEHAMA.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Erwan Gelebart, Mkurugenzi Mtendaji wa AXIAN Digibank & Fintech, amemshukuru Pesha kwa uongozi mahiri na mchango wake katika ukuaji wa Mixx kitaasisi, maendeleo endelevu na utekelezaji wa mikakati ya kampuni.

“Angelica amekuwa sehemu muhimu ya safari ya Mixx Tanzania. Kwa kiasi kikubwa, yeye pamoja na timu yake wameijenga biashara hii kutoka mwanzo hadi kuwa kampuni kubwa na mshirika anayeaminika katika maisha ya kila siku ya Watanzania,” amesema Gelebart.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Louis-Olivier Favot alijiunga na Mixx Tanzania akiwa na uzoefu wa miaka 17 katika sekta za benki, huduma ndogo za fedha, huduma za fedha kwa njia ya simu na huduma za kifedha za kidijitali. Kati ya hiyo, miaka 14 amefanya kazi katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Uzoefu wake unahusisha kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha, kubuni bidhaa, kuendesha biashara, kuboresha uzoefu wa wateja, kusimamia utoaji wa huduma na kutumia teknolojia kuboresha mifumo na huduma.

Kabla ya kujiunga na Mixx Tanzania, Favot alikuwa Afisa Mkuu wa Uendeshaji na baadaye Afisa Mtendaji Mkuu wa MVola, kampuni tanzu ya AXIAN inayotoa huduma za kifedha za kidijitali nchini Madagascar.

Uzoefu huo unamweka Favot katika nafasi nzuri ya kuongoza awamu inayofuata ya ukuaji wa Mixx Tanzania, huku akisaidia kupanua zaidi upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania.

Akizungumza kuhusu uteuzi huo, Gelebart amemkaribisha Favot Mixx Tanzania na kumtakia mafanikio katika nafasi yake hiyo mpya.“Louis-Olivier, karibu sana Mixx Tanzania! Nakutakia kila laheri na mafanikio katika nafasi yako mpya”.

Mabadiliko hayo ya uongozi yanafanyika wakati Mixx Tanzania ikiendelea kutekeleza azma yake ya kutoa huduma za kifedha zinazopatikana kwa urahisi, bunifu na zinazotumia teknolojia ya kidijitali kurahisisha upatikanaji huduma kwa gharama nafuu.