October 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UN:Mabunge yana nafasi kubwa kuharakisha Maendeleo 

Na Penina Malundo,TimesMajira

MRATIBU Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania, Susan Namondo, amesema mabunge yana nafasi kubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia utungaji wa sheria, upitishaji wa bajeti na usimamizi wa serikali.

Namondo ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaofanyika Arusha, akieleza kuwa mabunge yanaweza pia kusaidia kuvuka tofauti za kisiasa na kijiografia kupitia diplomasia ya kibunge.

Amesema wananchi wa mataifa mbalimbali wana mahitaji yanayofanana, yakiwemo elimu bora, huduma za afya na fursa za kiuchumi, hivyo mabunge yanapaswa kuhakikisha sauti zao zinafika katika maamuzi ya serikali.

Kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Namondo alisema mabunge yana jukumu la kuhakikisha malengo hayo yanaingizwa katika mipango na sera za kitaifa.

Hata hivyo, amesema utekelezaji wa SDGs bado ni changamoto duniani, kwani takribani asilimia 36 pekee ya malengo hayo ndiyo yaliyofikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa.

Amezitaka bunge kuimarisha usimamizi na uwajibikaji, ikiwemo kuchunguza matumizi ya fedha na kuhakikisha rasilimali za maendeleo zinatumika kwa ufanisi.