
Na Joyce Kasiki, Geita
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kazi kubwa ya kukusanya na kutunza takwimu zinazotumika katika kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya Taifa.
Sangu alitoa pongezi hizo leo Sept 24, 2026 alipotembelea banda la NBS kwenye Maonyesho ya Tisa ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yaliyoanza juzi mkoani Geita, akieleza kuwa takwimu sahihi ni msingi muhimu katika kufanya maamuzi na kupanga maendeleo ya nchi.
Alisema NBS inafanya kazi nzuri katika kuhakikisha Serikali na wadau mbalimbali wanapata takwimu zinazohitajika kwa ajili ya mipango na utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo mbalimbali.
“NBS wanafanya kazi nzuri, bila wao hakuna mipango inaenda,” alisema Sangu, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ukusanyaji, uchambuzi na utunzaji wa takwimu nchini.
Alisema takwimu zinazozalishwa na taasisi hiyo zina mchango mkubwa katika kusaidia Serikali kutambua mahitaji ya wananchi, kuweka vipaumbele na kupanga mikakati ya maendeleo yenye kuzingatia hali halisi ya Taifa.
Sangu ameitaka NBS kuendelea kuisadia Serikali kufikia malengo yake kwa kuhakikisha takwimu zinapatikana kwa wakati na zinatumika ipasavyo katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Taifa.
Aidha, alisema kazi hiyo ni muhimu katika safari ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inalenga kuweka msingi wa maendeleo endelevu na kuboresha maisha ya Watanzania.
Ameipongeza NBS kwa ushiriki wake katika Maonyesho ya Tisa ya Kimataifa ya Madini, akisema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi na wadau kupata uelewa kuhusu kazi zinazofanywa na taasisi hiyo pamoja na umuhimu wa takwimu katika sekta mbalimbali za uchumi

More Stories
Visima vya umwagiliaji vyawakomboa wakulima wadogo
PSSSF yapongezwa kwa mafanikio makubwa
Miradi ya kusambaza umeme vitongojini kukamilika ifikapo 2030