Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
KATIKA kuadhimisha Siku ya Faru Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Septemba 22, Ngoteya Wild imezindua filamu ya “The Rhinos of Ngorongoro – A Conservation Story”, inayotoa mtazamo wa ndani kuhusu maisha ya faru na juhudi zinazofanyika kila siku kuhakikisha wanyama hao wanaendelea kuwepo katika mazingira yao ya asili.
Filamu hiyo imeandaliwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ikiwa na lengo la kuonyesha umuhimu wa uhifadhi wa faru pamoja na mchango wa wataalamu na watendaji mbalimbali wanaohusika katika ulinzi na ustawi wa wanyama hao.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lina nafasi muhimu katika uhifadhi wa faru, likiwa miongoni mwa maeneo yanayohifadhi faru weusi na faru weupe. Kupitia filamu hiyo, watazamaji wanapata fursa ya kuona kwa karibu shughuli za ulinzi, ufuatiliaji na huduma za kitabibu zinazofanyika kuhakikisha faru wanakuwa salama na wenye afya.
Filamu hiyo haijaangazia faru pekee, bali pia imeibua simulizi ya watu wanaofanya kazi kuhakikisha wanyama hao wanaendelea kuwa sehemu ya mandhari ya Ngorongoro.

Miongoni mwa wanaoonekana katika kazi hiyo ni askari wa uhifadhi, wafuatiliaji wa wanyamapori (trackers) na madaktari wa wanyamapori, ambao kwa pamoja hutumia ujuzi, uzoefu na kujitolea kuwafuatilia, kuwachunguza na kuhakikisha usalama na afya ya faru.
Kazi hiyo inahusisha shughuli mbalimbali, ikiwemo kutambua alama za nyayo, kufuatilia mienendo ya faru na kuchunguza hali zao katika mazingira yao ya asili. Kwa mujibu wa simulizi ya filamu, shughuli hizi zinahitaji ushirikiano wa karibu, uvumilivu na uelewa mpana wa mazingira.

Filamu pia inaonyesha kuwa mafanikio ya uhifadhi wa faru hayawezi kutegemea kundi moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa askari wa uhifadhi, trackers, madaktari wa wanyamapori, wataalamu wa ikolojia, viongozi, jamii na wadau wengine.
Kwa mtazamo huo, uhifadhi wa faru unaelezwa kuwa ni jukumu la kizazi cha sasa kwa ajili ya vizazi vijavyo, huku Ngorongoro ikiendelea kuweka mkazo katika ulinzi, ufuatiliaji, utaalamu, matumizi ya teknolojia na ushirikishwaji wa jamii.
Muongozaji wa filamu hiyo ni Hans Cosmas Ngoteya, akishirikiana na Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na timu nzima ya Ngoteya Wild.
Kupitia “The Rhinos of Ngorongoro – A Conservation Story”, Ngoteya Wild inaleta karibu na watazamaji simulizi ya kile kinachotokea nyuma ya pazia katika kuhakikisha faru wa Ngorongoro wanaendelea kuwepo na kuwa sehemu muhimu ya urithi wa Tanzania na dunia.
Filamu hiyo sasa inapatikana kwenye YouTube kupitia akaunti ya Ngoteya Wild, ikiwa ni sehemu ya ujumbe wa kuhamasisha uelewa na umuhimu wa kuendelea kuwalinda faru na mazingira yao.

More Stories
OMTZD yakamilisha mipango ya kukabiliana na mafuriko Dar es salaam
Wananchi Matongo Mara kupata fidia
TPDC yadhamiria kufikisha gesi asilia viwandani