September 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanga yaweka mikakati kukabiliana na El-nino

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tanga

MKOA wa Tanga umeweka mikakati mahsusi ya kukabiliana na maafa yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa za El-nino,ambapo viongozi wa wilaya na wadau mbalimbali wametakiwa kuchukua hatua za haraka za tahadhari kabla ya mvua hizo kuanza na kuleta madhara kwa jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maandalizi ya mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amesema,mkoa huo umeunda timu tendaji ya kukabiliana na maafa inayojumuisha wadau kutoka taasisi mbalimbali, wakiweo Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), mamlaka za maji, sekta binafsi pamoja na taasisi nyingine za umma.

Aidha amesema,timu hiyo imepewa jukumu la kubaini maeneo hatarishi na kuchukua hatua mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza endapo mvua zitanyesha kwa kiwango kikubwa.

Amesema miongoni mwa hatua zilizowekwa ni kubaini maeneo salama ambayo yanaweza kutumika kuwahifadhi wananchi watakaoweza kuathirika na mafuriko au majanga mengine, pamoja na kufanya usafi na kuzibua mifereji, mitaro, makalavati na madaraja yanayoweza kuziba na kusababisha maji kushindwa kupita.

Aidha, maeneo ambayo yamewahi kukumbwa na changamoto wakati wa mvua yanaendelea kufanyiwa tathmini, huku hatua za kujenga au kuboresha makalavati zikichukuliwa pale inapohitajika.

Balozi Dkt. Burian amesema,Wakuu wa Wilaya zote wamepewa jukumu la kufanya tathmini katika maeneo yao na kuhakikisha maandalizi yanafanyika mapema ikiwemo kusafisha mitaro na kuondoa taka zinazoweza kuziba njia za maji.

Kwa upande wa barabara kuu zinazosimamiwa na TANROADS amesema, maeneo yanayokusanya maji yanaendelea kutambuliwa ili kuweka mikakati ya kuyaondoa na kuzuia kutokea kwa mafuriko yanayoweza kuathiri usafiri na shughuli za wananchi.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amesema,maandalizi yamejumuisha pia mikakati ya kudhibiti magonjwa ya milipuko ambayo yanaweza kujitokeza baada ya mafuriko, ikiwemo kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa endapo mlipuko wa ugonjwa utatokea.

Pia amesema,maandalizi hayo yanafanyika kwa uratibu wa mkoa na wilaya zote ili kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kutolewa hata wakati wa maafa.

Aidha amesisitiza kuchukuliwa kwa hatua za udhibiti katika shughuli za madini pale zinapoweza kuongeza hatari ya maafa wakati wa mvua kubwa, huku mamlaka husika zikielekezwa kusimamia utekelezaji wa hatua hizo kwa lengo la kulinda maisha na mali za wananchi.

Kwa upande wa sekta ya uvuvi amesema, mkoa umeimarisha utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa wavuvi ili kuwawezesha kuchukua tahadhari kabla ya kwenda baharini.

Hata hivyo amesema,hatua hiyo ni muhimu hasa wakati hali ya hewa inapokuwa mbaya, kwa kuwa vyombo vidogo vya uvuvi vinaweza kukumbwa na mawimbi makubwa na kusababisha madhara.

Sanjari na hayo amesema,maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha Mkoa wa Tanga haukusubiri maafa yatokee ndipo uchukue hatua, bali unatambua mapema maeneo yenye hatari, kuimarisha miundombinu na kuwaandaa wananchi pamoja na taasisi zote zinazohusika kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.