Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
WATAALAMU na mabingwa wa afya kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wanatarajiwa kusafiri ndani ya treni ya SGR kuanzia Septemba 21 hadi 27, mwaka huu, kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza kwa abiria watakaopenda kupimwa.
Huduma hizo zitatolewa bure kupitia ushirikiano kati ya JKCI na Shirika la Reli Tanzania (TRC), ukiwalenga abiria wanaosafiri kwa treni ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma, kuelekea maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yanayofanyika kila mwaka Septemba 29.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Septemba 18, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema huduma hizo zitahusisha vipimo vya Echo, ECG, sukari na mafuta kwenye damu.
Amesema vipimo hivyo vikitolewa hospitalini vinaweza kugharimu zaidi ya Sh500,000, lakini katika wiki hiyo ya afya ya moyo abiria watapata huduma hizo bila malipo wakiwa safarini.

“Kwa kipindi hiki chote cha wiki ya afya ya moyo, abiria wote watapata huduma hizi bure kabisa wakiwa safarini,” amesema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Machibya Kadogosa amesema ushirikiano huo ni mwanzo wa mpango mkubwa zaidi wa kimkakati, ambapo TRC ipo katika hatua za usanifu wa kutengeneza mabehewa maalum yatakayokuwa na vifaa vya matibabu na vitanda.
“Mabehewa haya yatasaidia sana kupunguza muda wa kusafirisha wagonjwa waliopo kwenye hali mbaya kutoka mikoani kama Dodoma na Morogoro kulinganisha na kutumia magari ya dharura (ambulance) ya barabarani”amesema
Aidha ametoa wito kwa wananchi na abiria watakaosafiri na SGR katika wiki hiyo kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo kupima na kuchunguza afya zao.

More Stories
TMDA yawanoa wataalam Kibaha kuhusu Dawa za kulevya
TMDA yaonya kuhusu chanjo bandia ya mifugo sokoni
Dc.Kilosa aagiza kudhibiti uvujaji mapato