Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Tanga
SERIKALI imetenga kiasi cha sh. bilioni 10 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa meli mpya ya mizigo itakayohudumia usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na nchi jirani kupitia Bahari ya Hindi.
Hatua hiyo inayolenga kuongeza uwezo wa usafirishaji wa majini na kuchochea biashara, uwekezaji na ajira hapa nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian amesema hayo wakati wa kikao na waandishi wa habari jijini Tanga, ambapo alitoa taarifa rasmi kuhusu maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani yatakayofanyika mkoani humo kitaifa kuanzia Septemba 21 hadi 24, 2026.
Amesema,uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya usafiri majini, ikiwemo kuboresha miundombinu ya bandari, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria, kuimarisha usalama wa vyombo vya majini, pamoja na kuongeza uwezo wa utafutaji na uokoaji.
Kwa mujibu wa Balozi Dkt.Burian, Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) imekamilisha utafiti wa mahitaji ya soko katika mwambao wa Bahari ya Hindi, ambao umewezesha kubaini mahitaji na aina ya meli inayofaa kujengwa kwa ajili ya kuimarisha usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na nchi jirani.
Amesema,hatua hiyo inalenga kuongeza nafasi ya usafiri wa majini katika kurahisisha biashara na usafirishaji wa bidhaa, huku ikitarajiwa kutoa fursa zaidi katika sekta mbalimbali zinazohusiana na uchukuzi wa majini.
Pia amesema,katika Mko wa Tanga Serikali imeendelea kufanya maboresho katika Bandari ya Tanga, hatua ambayo imeongeza ufanisi wa huduma za bandari na kuchochea ongezeko la shughuli za usafirishaji wa mizigo pamoja na kuongezeka kwa meli zinazofika katika eneo hilo.
Hata hivyo amesema,maendeleo hayo yanaifanya sekta ya usafiri majini kuwa sehemu muhimu ya kuchochea shughuli za kiuchumi mkoani Tanga, ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii na ajira, kutokana na nafasi ya mkoa huo katika mwambao wa Bahari ya Hindi.
Sanjari na hayo amesema,Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya usafiri majini sambamba na kuongeza usalama wa vyombo na abiria wanaotumia usafiri huo huku sekta hiyo imeendelea kuhusisha zaidi sekta binafsi katika uendeshaji na uendelezaji wa shughuli za bandari na huduma za usafiri majini, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kuchochea uwekezaji.

Hata hivyo amesema,kilele cha maadhimisho Siku ya Usafiri Majini Duniani kinatarajiwa kufanyika Septemba 24, 2026, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, wakati shughuli za awali zikitarajiwa kuhudhuriwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Khalid Mohamed.
Kwa ujumla, Serikali inaendelea kuweka msisitizo katika kuimarisha usafiri wa majini kama sehemu ya kuongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo na abiria, kukuza biashara na uwekezaji pamoja na kufungua fursa za ajira, huku Tanga ikiwa miongoni mwa mikoa yenye nafasi muhimu katika utekelezaji wa jitihada hizo kutokana na uwepo wa bandari na mwambao wa Bahari ya Hindi.

More Stories
Tanga yaweka mikakati kukabiliana na El-nino
Ndejembi aungana na wananchi kufanya mazoezi.
JKCI kupima Afya za Abiria SGR bure