Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
SHIRIKA la kuteta haki za wanawake na watoto Kivulini,husaidia kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia,familia salama,wanawake na vijana waliowezeshwa fursa za kiuchumi na uwezo wa jamii kujiletea maendeleo yenyewe.
Ambapo shirika hilo limechangia maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza kwa kukuza uwezeshaji wa kiuchumi, kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na Serikali,kuanzisha vikundi malezi zaidi ya 40 pamoja na kuwajengea uwezo wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Hayo yameelezwa Septemba 14,2026 na Mkurugenzi wa shirika la Kivulini Yassin Ally katika maadhimisho ya kilele cha mwezi wa Maendeleo ya Jamii,ambapo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela yamefanyika eneo la Kontena Kata ya Nyamanoro,yalioambatana na kliniki maalum ya maendeleo ya jamii yakiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu ushiriki wa jamii katika shughuli za maendeleo na kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050, chini ya kaulimbiu “Familia Imara, Uchumi Imara, Taifa Imara”.
Ally amesema,Kivulini imehamasisha na kuchangia maendeleo ya jamii kwa kujenga Soko la Kiloleli lililopo katika halmshauri hiyo pamoja na kituo cha kunyonyeshea na choo cha kisasa katika soko hilo vyenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 200.
“Tumeijengea uwezo taasisi moja ya wasaidizi wa kisheria ngazi ya Wilaya yenye wasaidizi 25Tumetoa ruzuku ya zaidi ya sh.milioni 30, ambazo zimewezesha kufikia watu zaidi ya 45,000 kwa njia ya elimu ya kisheria ambapo wanawake na wasichana zaidi ya 700 wamepata msaada wa kisheria bure kupitia wasaidizi wa kisheria Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,”amesema Ally.
Vilevile amesema, shirika hilo limeanzisha vikundi malezi 20 vyenye jumla ya wanakikundi 560 katika halmshauri hiyo vinavyowezeshwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwenye masuala ya lishe,malezi,ukatili dhidi ya wenzake na watoto pia kuhamasisha maendeleo ya jamii ili kuwa na familia na jamii zenye ustawi.
Sanjari na hayo amesema,shirika hilo limeijengea uwezo na kuimarisha ujasiri wa wanawake na wasichana kushiriki katika mambo ya uongozi,maamuzi,kudai haki zao na akimtolea mfano Diwani wa Kata ya Nyamh’ongolo Safia Mkama ambaye ni mnufaika na kwa mara ya kwanza ameshika nafasi hiyo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya
Nyamh’ongolo Safia Mkama amesema,alipikwa na shirika hilo tangu mwaka 2011 akiwa Mwenyekiti wa UWT Kata,Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Mwenyekiti UWT Wilaya ya Ilemela,Diwani wa Viti Maalumu mara mbili na sasa ni Diwani kamili wa Kata hiyo.
“Juhudi hizi zimetoka katika shirika zimemjengea uwezo wa kujiamini, kusimamia na kupambana na wakina baba.Uchaguzi wa mwaka jana haukuwa mwepesi lakini nikasimama na Mungu akasimama nikashinda.Kivulini wakina mama wanahitaji mikubwa endeleeni kuwasaidia ili waweze kushiriki katika nafasi za uongozi,”amesema Mkama
Naye Katibu wa Soko la Kiloleli Maximilian Kishankala amesema,shirika la Kivulini limekuwa chachu ya maendeleo ambapo wameweza kupata choo chenye matundu 10,jengo la mama na mtoto na jengo la wauza mbogambiga.Hivyo ameliomba kuendelea kuliona soko hilo kama sehemu ya kufanyia kazi ili Watanzania wengi waweze kupata huduma kwani mpaka sasa kuna wafanyabiashara wapatao 2000 na linatarajia kuwa na wafanyabiashara zaidi ya 5000.


More Stories
OMDTZ yawezesha wananchi mipango kukabili mafuriko
Mradi wa Mawasiliano waongeza ufanisi huduma za Serikali
TALGWU kufanya Mkutano Mkuu kupitia taarifa ya maendeleo