September 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kijana apigwa risasi tuhuma za uhalifu benki

Na Judith Ferdinand,Mwanza 

KIJANA  mmoja anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 35,amefariki kwa kupigwa risasi kwa tuhuma za kuingia benki kwa nia ya kutenda uhalifu.

Akizungumza Septemba 14,2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbord Mutafungwa amesema,Septemba 13,2026, majira ya saa 7:58 mchana,walipokea taarifa ya tukio la mtu mmoja wa jinsia ya kiume anayekadiriwa kuwa na miaka 30 hadi 35, ambaye bado hajafahamika jina wala makazi, inadaiwa aliingi ndani ya Benki ya CRDB, Tawi la Rock City Mall,Wilaya ya Ilemela mkoani humo, kama mteja na kuwalazimisha wahudumu wa benki hiyo wampatie fedha.

DCP.Mutafungwa amedai kuwa mtu huyo aliyekuwa amevaa kofia aina ya kapero, shati la mikono mirefu,suruali ya “jeans” yenye rangi nyeusi na viatu vya wazi, baada ya kufika sehemu ya kutolea huduma kwa wateja, alimuomba mhudumu ampatie fedha ya kula. 

Amesema,mhudumu alimpa utaratibu wa kutoa na kuweka fedha, lakini mtu huyo aliendelea kusisitiza apewe fedha ya kula.Katika hali hiyo, mhudumu alihisi hali ya hatari, hivyo aliamua kwenda kwa wafanyakazi wenzake ili kupata msaada.

“Mtuhumiwa naye aliruka kaunta ya sehemu ya kutolea huduma kwa wateja na kuelekea moja kwa moja kwenye vyumba vya kuhesabia fedha, kisha kumsukuma mhudumu na kuingia naye sehemu ya chumba cha kuhesabia fedha.Kitendo hicho kilizua hofu na kuleta taharuki kubwa kwa wafanyakazi na wateja waliokuwa wanapata huduma za kibenki,”ameeleza DCP.Mutafungwa.

Pia amesema,baada ya kitendo hicho Askari wa Jeshi la Polisi ambao hutoa huduma ya ulinzi katika benki hiyo mara moja walifika kutoa msaada, hivyo walimtaka mtuhumiwa kujisalimisha mikononi mwa polisi, lakini mtu huyo aliamua kukaidi amri hiyo halali na kuanza kupambana na askari kwa kujaribu kuwasogelea na kutaka kuwanyang’anya silaha, huku akikaidi amri ya kujisalimisha na kukaa chini.

Kutokana na hali hiyo, Mutafungwa amedai kuwa askari walibaini kuwa mtu huyo hakuwa na nia njema, hivyo waliamua kumdhibiti kwa kumpiga risasi kiunoni upande wa mguu wa kulia na kumsababishia jeraha lililosababisha kuvuja damu nyingi na wakati anakimbizwa hospitali alibainika kuwa amepoteza maisha. 

Ametaja chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya fedha aliyokuwa nayo mtuhumiwa hivyo mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure kwa ajili ya utambuzi na hatua nyingine za uchunguzi. 

Hata hivyo amesema,marehemu alipofanyiwa upekuzi kwenye maungo yake, alikutwa na simu moja aina ya Samsung rangi nyeusi na pesa kiasi cha shilingi mia tano.Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na linatoa onyo  dhidi ya vitendo vya uhalifu na halitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote watakaoendelea kuvunja sheria.