September 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpanju atoa wito wadau kuimarisha Mabaraza ya watoto

Na Zena Mohamed,TimesMajira Online,Dodoma

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum,Wakili Amon Mpanju, amewataka wadau wa maendeleo hususani wanaojishughulisha na watoto, kugawana maeneo ya kufanyia kazi badala ya kujikita eneo moja.

Mpanju amesema hayo jijini hapa leo Septemba wakati akizindua kanuni za uanzishaji, uendeshaji na uratibu wa Mabaraza ya Watoto nchini ambapo amesema, matarajio ya Serikali ni kuzindua Mabaraza ya watoto nchi nzima, hivyo ni vema wadau kupeana maeneo tofauti ili kurahisisha uratibu wa mabaraza hayo kwenye kila eneo.

“Isiwe ni maneno ya Jukwaani tu, tufanye “mapping” (ramani) ili kujua nani anafanya nini na wapi kuhakikisha utekelezaji wa mabaraza unafanyika kwa ufanisi, kuanzia uanzishwaji, uendeshaji, ufuatiliaji na Tathmini. Lengo la mabaraza ni kuendeleza watoto wetu, kujua haki zao, kutambua vipaji vyao na kuwaandaalia kesho yao,”amesema Mpanju.

Aidha, amewaelekeza watendaji kuanzia ngazi ya Wizara kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuhakikisha Mabaraza ya Watoto yanaanzishwa na wadau wanakuwa na ramani ya namna ya kuratibu utendaji kazi wa mabaraza hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watoto Daniel Magembe, ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha mabaraza ya watoto yanatambulika kisheria na ameomba kuzingatiwa kwa utengaji wa bajeti katika utekelezaji wa majukumu ya mabaraza hayo.

Magembe amesema mapendekezo mbalimbali yaliyojadiliwa na Kamati Kuu ya Baraza la Watoto, ikiwemo kuboreshwa kwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 hasa eneo la umri wa kuolewa na maboresho ya miundombinu inayoendana na wakati wa sasa.

Mkurugenzi wa kitengo cha Sheria, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Msomi Dereck Mwajombe, amesema marekebisho mbalimbali ya sheria ya mtoto yamefanyika ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto unaimarishwa.

Akitaja baadhi ya marekebisho hayo Mwajombe amesema ni pamoja ma Sheria ya makosa ya Mtandaoni, Sheria ya mtoto eneo la uchepushaji yaani mtoto aliyekinzana na sheria kuwa na nafasi ya kurekebishwa badala ya kukaa gerezani pamoja na uundwaji wa mabaraza ya watoto kuwa kwenye mfumo wa Kisheria.

Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Watoto, Maadili na Malezi Asha Vuai, amesema mtoto anapopewa nafasi ya kusikilizwa na kuhirikishwa anakuwa na kuelewa kwamba yeye ni shemu ya jamii na mawazo yake yana thamani kwenye jamii.

“Tunapozungumzia mabaraza ya watoto, hatuzunguzii tu mkutano kama huu wa leo, isipokuwa tunazingumza mambo mbalimbali yanayowahusu watoto ambao ni pamoja mfumo unawajenga watoto kujieleza, kusikilizwa, kujifunza uongozi na kuelewa nafasi zao katika famili, jamii na Taifa kwa ujumla,”amesema.

Jukwaa hilo limeandaliwa na Tanzania Child Rights Forum (TCRF) kwa kushirikiana na Mashirika mengine ikiwemo Save the Children Tanzania.