Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tabora
KILA mtumishi aliyepewa dhamana ya kutumikia wananchi ndani ya Serikali mkoani Tabora ametakiwa kuwa mstari wa mbele kusikiliza na kutatua kero zao na sio kusubiri hadi viongozi wa ngazi za juu wafanye ziara katika eneo lao.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Benno Malisa alipokuwa akiongea na viongozi mbalimbali wakiwemo watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tawala wa Wilaya na wengineo.

Amesisitiza kuwa viongozi au watumishi hawakuajiriwa ili wakae ofisini tu kwenye kompyuta, bali kutembelea maeneo ya wananchi ili kujionea miradi inayotekelezwa, kusikiliza kero zao na kuangalia namna ya kuwasaidia.
Pia ameagiza viongozi na watendaji wa ngazi zote kuanzia mitaa,vijiji,kata,wilaya hadi mkoa kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa wananchi ili kupunguza malalamiko na kero zinaikabili jamii katika maeneo hayo.
“Viongozi wa dini pia mna dhamana ya kusikiliza changamoto zinazowakabili waumini wenu na kuzitafutia ufumbuzi ili jamii iendelee kuishi kwa amani,utulivu na kumwabudu Mungu vizuri,”amesema Malisa na kuongeza:
“Suala la kutatua kero za wananchi ni jukumu letu sote,tulibebe kwa pamoja na kila mmoja katika nafasi yake asikilize na kuzitatua, katika hili nahitaji sana ushirikiano wenu wa kutosha, ofisi yangu itakuwa wazi masaa 24,”.
Hata hivyo amesema,wananchi wanataka maendeleo ndiyo maana serikali imeendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji miradi mbalimbali, hivyo akaelekeza isimamiwe ipasavyo na kama kuna kero itatuliwe.
Akiongea katika kikao hicho Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Ghullam- Dewj amesema,watampa ushirikiano wa kutosha Mkuu wa Mkoa huyo.


More Stories
Twenzetu kileleni kuhamasisha utalii wa ndani
QNET yaimarisha uongozi,Tanzania yawekwa kipaumbele
Tuzo za Wafugaji kuongeza tija ya Mifugo