September 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SAPP yafungua fursa Tanzania kuwa kitovu cha umeme

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira

MIKUTANO ya 67 ya Jumuiya ya Umeme ya Kusini mwa Afrika (SAPP) inayofanyika Zanzibar imefungua fursa mpya kwa Tanzania kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha biashara ya umeme katika ukanda wa Kusini mwa Afrika, huku ikitarajiwa kuongeza mapato ya taifa kupitia mauzo ya umeme na kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda huo.

Mikutano hiyo imewakutanisha wajumbe kutoka nchi wanachama 18 wa SAPP kwa lengo la kujadili masuala ya biashara ya umeme, uendeshaji wa mifumo ya umeme, uwekezaji katika miundombinu ya nishati na usalama wa nishati katika nchi zilizoko ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Akifungua mikutano hiyo Septemba 8, 2026 katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar, Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Bw. Haji Mohamed Haji, amesema kuimarishwa kwa uunganishaji wa gridi za umeme kati ya nchi wanachama kutarahisisha biashara ya umeme kuvuka mipaka na kuwezesha nchi zenye ziada ya umeme kuziuzia nchi zinazokabiliwa na upungufu wa nishati.

Amesema ushirikiano huo utaongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali za nishati zilizopo katika ukanda, kupunguza gharama za uzalishaji wa umeme na kuimarisha uthabiti wa mifumo ya umeme.

“Kwa kuunganisha mifumo ya gridi za taifa na kuwezesha biashara ya umeme kuvuka mipaka, nchi za SADC zitaweza kupunguza changamoto za upungufu wa umeme, kuimarisha uthabiti wa gridi na kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi,” amesema Haji.

Kwa Tanzania, mikutano hiyo inafanyika wakati nchi ikiwa imeongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wake wa kuzalisha umeme kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) uliokamilika pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya usafirishaji wa umeme inayounganisha maeneo mbalimbali ya nchi na nchi jirani.

Ongezeko hilo la uzalishaji wa umeme linaipa Tanzania nafasi ya kunufaika zaidi na soko la kikanda la umeme kwa kuuza ziada ya nishati katika nchi wanachama wa SAPP, hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya taifa, kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SAPP, Mhandisi Stephen Dihwa, amesema mikutano hiyo ni jukwaa muhimu la nchi wanachama kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano wa kiufundi na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, nafuu na endelevu katika ukanda.

“Mikutano hii inatoa fursa kwa kamati mbalimbali za kitaalamu za SAPP kuwasilisha kazi zao, kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta ya umeme. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi katika ukanda wa Kusini mwa Afrika wanapata umeme wa uhakika, unaopatikana kwa gharama nafuu na unaozingatia uendelevu,” amesema Dihwa.

Mikutano hiyo inayofanyika kuanzia Septemba 7 hadi 11, 2026 inatarajiwa kutoa maazimio yatakayosaidia kuimarisha biashara ya umeme kati ya nchi wanachama, kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji wa umeme na kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda.

Kwa Tanzania, maendeleo hayo yanatajwa kuwa hatua muhimu katika safari ya kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza biashara ya umeme barani Afrika, huku yakifungua fursa za kuongeza mapato ya fedha za kigeni, kuimarisha usalama wa nishati na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya taifa.